RC Babu alivyotinga hospitalini kimyakimya na mgonjwa, abaini ‘madudu’

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Nurdin Babu amesikitishwa na huduma mbovu zinazotolewa na baadhi ya wahudumu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mawenzi, mkoani humo.

Hatua hiyo inatokana yeye kumpeleka mgonjwa hospitalini hapo na kupewa huduma isiyoridhisha ambayo aliisubiri kwa zaidi ya saa tatu.

RC Babu amesema alikwenda hospitalini hapo akiwa amevalia kanzu na kofia kama mwananchi wa kawaida na wahudumu hao hawakutambua kama ni mkuu wa mkoa huo.

Kiongozi huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo jana, Agosti 12, 2025 wakati akizungumza katika kikao cha tathimini ya hali ya lishe kwa mwaka 2024/2025 kwa Mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano wa mkoa huo.

“Unakwenda hospitali unakuta mhudumu wa afya anachezea na simu, hana hata kalamu ya kuandikia, mnakasirisha sana nyie, lakini nataka nikwambie (RAS).

“Rais anaweza akapewa lawama kwa sababu yetu sisi, haki ya Mungu nakwambia, Mkuu wa Mkoa? au kwa vile nimevaa kanzu na kofia? hili ni vazi tu kama vazi lingine, siwezi kuvaa kaunda suti wakati wote,” amesema RC Babu

“Aisee nilikasirika, nikawapigia wakaja madaktari sita sijui akaja ‘supervisor’ sijui nani, sasa kama mkuu wa mkoa anafanyiwa hivyo raia wa kawaida?, haki ya Mungu ile siku sikulala usiku kucha nilikuwa nimekasirika sana na yule dada namkumbuka baba yake angekufa yaani tungesumbuana vibaya sana.”

RC Babu amesema mgonjwa anapopelekwa idara ya dharura na kudaiwa fedha ya ajili ya matibabu, kwanza sio jambo zuri anapaswa kupokewa kwanza na kupatiwa huduma ya haraka kuokoa maisha yake na sio kuweka mbele masuala ya fedha.

“Halafu mtu anapelekwa ’emergency’, mtu hawezi kutoroka, anaumwa (halafu) wanasema hawezi kupigwa sindano au kutibiwa mpaka aende kule alipe fedha, aiseee halafu mtu anakata roho mnafanyaje hela yenyewe Sh10,000, Sh13, 000 nimelipa 72,000 tuu pale,” amesema RC Babu

Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS), Yusuf Nzowa kufuatilia utendaji kazi wa wahudumu wa afya wa hospitali hiyo.