Rushwa, umri mkubwa vyakatisha tamaa vijana kuwania uongozi

Butiama. Baadhi ya vijana katika Mkoa wa Mara wameeleza kuwa ukosefu wa fursa za kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa ni miongoni mwa sababu zinazowakwamisha vijana wengi kushiriki katika upigaji kura kwenye chaguzi mbalimbali.

Wamesema mara nyingi nafasi za uongozi wa kisiasa hupewa watu wenye umri mkubwa (wazee) au wale waliokaa madarakani kwa muda mrefu, hali inayowakatisha tamaa vijana na kuwafanya kuona hakuna nafasi kwao ndani ya mifumo ya kisiasa.

Vijana hao wametoa maoni yao leo, Agosti 13, 2025, katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika wilayani Butiama.

Wamesema kuwa hata pale wanapojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa kisiasa, wengi wao hukatishwa tamaa na changamoto kama vile vitendo vya rushwa na upendeleo.

Pia, wamesisitiza kuwa ili kuongeza ushiriki wa vijana katika mchakato wa kidemokrasia, ni muhimu kuwajengea mazingira rafiki, yanayowapa nafasi sawa ya kushiriki katika siasa na uongozi.

“Suala la vijana kutokupiga kura ni janga la Taifa, imefika hatua vijana hawaoni sababu ya kupiga kura, kwani wanaona wanapoteza muda badala yake wakati wa kupiga kura wanakuwa wanafanya mambo yao, hii hali sio nzuri inatakiwa kupatiwa ufumbuzi,” amesema Ibrahim Richard.

Kwa upande wake Musa Mkiranda amesema ushiriki wa vijana unakuwa mkubwa pale ambapo vijana wenzao wanapopata fursa hiyo, hivyo kupendekeza kuwa mchakato wa uchaguzi  kuanzia ngazi ya vyama vya siasa unatakiwa kuwa huru na haki.

“Kama hauamini subiri wakati wa uchaguzi uje uone, sehemu ambazo kuna wagombea vijana, utaona vijana wengi wanajitokeza kupiga kura, hii ina maana kuwa vijana ambao ndio idadi kubwa ya Watanzania wanataka wawakilishi wanaotokana na wao,” amesema.

Amesema vijana wengi wanakata tamaa ya kupiga kura kutokana na mazingira wanayokutana nayo wenzao wanaothubutu kugombea, kwani wengi wao wanakuwa hawana fedha, jambo ambalo linatumiwa na wagombea wengine kujipatia ushindi.

“Mimi mwenyewe nimegombea kipindi hiki, nilichokutana nacho ni siri yangu kwa hiyo vijana wanaona kupiga kura kuchagua viongozi wale wale waliodumu kwenye nafasi hizo kwa zaidi ya miaka 20 ni kupoteza muda, bora wakajitafutie riziki,” amesema Mkiranda.

Pia, Vaileth Joseph amesema baadhi ya vijana wamekuwa wakipuuzia upigaji kura kwa kuwa wanaamini hawana wajibu katika mchakato huo wa kidemokrasia.

Hivyo, amesisitiza kuwa kuna haja ya kuendelea kutoa elimu na hamasa zaidi ili kuongeza ushiriki wa vijana katika uchaguzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Power Life, Kaijage Novatus, amesema ushiriki mdogo wa vijana katika upigaji kura ndiyo moja ya sababu zilizochochea kuandaliwa kwa kongamano hilo.

Novatus amesema suala hilo linahitaji uwajibikaji wa pamoja kutoka kwa jamii nzima, ili kuweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki na kuwachagua viongozi wanaowakilisha matakwa yao.

“Suala la vijana kupiga kura linahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali katika jamii kuanzia familia, dini, elimu na kila mmoja wetu ili vijana waone umuhimu wao wa kushiriki kwenye kuchagua viongozi kwa masilahi ya jamii na taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema ni wajibu wa jamii nzima kuwatengengeza vijana ili waone umuhimu wao kwenye masuala muhimu ya taifa, likiwepo suala la uchaguzi kwa ujumla.

Kongamano hilo lililoshirikisha vijana zaidi ya 300 kutoka katika wilaya sita za Mkoa wa Mara, mbali na kuangazia suala la ushiriki wa vijana kwenye chaguzi, pia limejadili namna vijana wanavyoweza kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya mkoa huo.