Salum Mwalimu amtaja Maalim Seif akiomba kuungwa mkono na Wazanzibari

Unguja. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ametembelea nyota ya kisiasa ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani, Maalim Seif Shariff Hamad akiomba kuungwa mkono na Wazanzibari kwenye mbio zake za urais.

Maalim Seif ambaye kwa sasa ni marehemu ni mwanasiasa aliyekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za Wazanzibari kwa nyakati zote alizogombea urais kuanzia Chama cha Wananchi CUF na baadaye alihamia chama cha ACT-Wazalendo na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) hadi alipofariki dunia Februari 17, 2021.

Salum Mwalimu huku akieleza dhamira yake ya kufuata nyayo za mwanasiasa huyo mkongwe katika harakati za kuleta mabadiliko na haki Zanzibar, wamewaomba Wazanzibari wamdhamini na kumpa kura.

Mwalimu kwenye mkutano wake huo amewaeleza Wazanzibari kwamba wana haja ya kutembea kifua mbele, kwani chama hicho kinakwenda kuleta mageuzi kisiwani humo huku akitaja kupitia kwenye nyayo za Maalim Seif Shariff Hamad.

Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Agosti 13, 2025 katika uwanja wa Mpendae wakati akizungumza na mamia ya wanachama na wananchi kwa ajili ya kujitambulisha na kuomba udhamini akiwa ameongozana mgombea mwenza, Devotha Minja.

Mwalimu alikabidhiwa fomu za kuwania urais na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi  (INEC) jana Agosti 12, 2025 makao makuu ya Tume hiyo Dodoma.

“Hamtajuta kunichagua mimi kwa sababu nimezaliwa Zanzibar, nikalelewa Zanzibar na kukulia Tanganyika, kwa hiyo najua mahitaji ya pande zote mbili, hivyo mimi ni mtu sahihi wa kuwapa haki sawa bila kuyumba wala kuyumbishwa,” amesema Mwalimu

Amewataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kutembea kifua mbele kwa sababu umefika wakati wa kuleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo na kifikra.

Mwalimu ambaye alikuwa Chadema, amesema iwapo kuna watu wanadhani ndoto za Maalim Seif Sharrif Hamad zimekufa watakuwa wanajidanganya kwa sababu anajua nia thabiti aliyokuwa nayo kiongozi huyo kwa hiyo anakwenda kuyatekeleza.

“Huyu Mzee wetu Maalim Seif hatuko naye kimwili, lakini bado fikra zake, ndoto zake na maono yake tunaviendeleza, na mimi naomba niwaahidi kwamba yote aliyolenga kuyafanya Maalim nitakwenda kuyatekeleza, wanaodhani yamekufa watasubiri sana,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwalimu, wataifanya Zanzibar kuwa sehemu salama, yenye upendo kama ilivyokuwa iwapo wakiwa na chaguo sahihi.

Mwalimu amesema katika maisha yake yote hajawahi kufanya kazi serikalini na amejenga heshima ya jina lake sio kupitia mgongo wa Serikali, hivyo anaamini hata akienda Ikulu hatakuwa na deni na mtu badala yake atakuwa na muda kuhakikisha anawatumikia wananchi.

“Kwa hiyo deni nitakalokuwa nalo ni kuwaletea wananchi maendeleo na kutatua changamoto zao, sina mtu ambaye amenibeba kwa hiyo hata nikiwa Ikulu sitahitaji kulipa fadhila,” amesema.

“Naomba mnikumbuke kwenye maombi yenu maana shughuli tunayokwenda nayo Oktoba 29 sio ndogo na baada ya hapo kasi itakuwa kubwa sana.

“Kila mara wanakuja kwetu kuomba kura wakienda Ikulu hawatukumbuki sasa tumeamua kwenda sisi ili kutengeneza ajira na vipato vyetu.

“Ikulu inahitaji akili, akili tunazo, Ikulu inahitaji utashi, utashi tunao kwa hiyo wacha twende Ikulu tuone kama haya yatatushinda,” amesema.

Naye Yericko Nyerere amesema wakati ndio huu chama hicho kimekuja kuwakomboa kwani kinajua changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake James Mbowe amesema wapo kwenye siasa za upinzani muda mrefu sio kwa sababu ya kutaka ulaji badala yake wanataka kutatua changamoto za wananchi na ajenda waliyokuwa nayo Chadema ndio wanayokwenda nayo Chaumma.