Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya OpenAI, inayomiliki programu ya akili unde Chatbot ya ChatGPT imekuja na sasisho jipya (New Update) lenye kipengele chenye uwezo wa kufikiri pia kufanya vitendo kwa niaba ya mtumiaji.
Kupitia toleo hilo jipya watumiaji sasa wanaweza kuitegemea katika kufikiri na kuchukua hatua ikiwa ni sehemu ya kusaidia watu sehemu ya ushindani na kampuni ya Google inayomiliki Gemini inayotajwa kutenda kwa ufanisi zaidi.
Kupitia taarifa iliyochapishwa katika ukurasa rasmi wa OpenAI na CNN, sasa mtumiaji anaweza mfano akaiomba ChatGPT kuangalia na kukagua kalenda yake kisha imwambie taarifa za mikutano yake ya mwezi ujao au wakati ujao, au uvae nguo gani kwenye sherehe kama harusi au utumie viungo gani kupika chakula kulingana na idadi ya watu.
Ikumbukwe watakaokuwa na uwezo wa kutumia sasisho hilo jipya ni wale waliojisajili kwenye ChatGPT Pro, Plus au Team.
Wakati hayo yanaendelea teknolojia ya AI, inaendelea kushughulika na mapungufu iliyonayo ikiwemo masuala ya faragha. Mifumo ya AI bado inakabiliwa na udanganyifu na upendeleo na inaweza kufanya jambo pasipo kutabiriwa.
ChatGPT sasa inaweza kufanya hivyo kutokana na kipengele hicho kipya cha o1 kilichotengenezwa ili akili unde hiyo iweze kufikiri, kufanya maamuzi sawa na binadamu.
Kipengele cha o1 ni uwezo wa kujibu maswali kwa kufuata mnyororo wa hoja, jambo ambalo ChatGPT ya awali ilishindwa.
Kwa mfano, ikiwa utauliza: “Mama yake Tom Cruise ni nani?” (jibu: Mary Lee Pfeiffer) kisha uulize tena “Mtoto wa Mary Lee Pfeiffer ni nani?” jambo ambalo awali ilikuwa ikipata shida kujibu. Lakini kwa sasa inaweza kujibu kwa usahihi na kuonesha hatua za kufikiri ilizopitia.
Lakini, hata hivyo bado kuna mashaka. Wataalamu wa eneo hili wanasema kauli kwamba o1 inafikiria ni ya kimasoko zaidi kuliko uhalisia wa kisayansi.
Kwa upande mwingine OpenAI imekiri ujio huo unaweza ukaleta hatari mpya huku ikisema imepunguza uwezo wa taarifa ambao mfumo unaiweza kuifikia, mfano kutuma barua pepe ambapo inahitaji uwepo wa msimamizi wa mtumiaji.
Pia mfumo huo umetakiwa kukataa kazi zenye hatari kubwa kama vile kuhamisha pesa benki kwa mujibu wa Sam Altman Mkurugenzi Mtendaji wa OpenAI.
Ameshauri watumiaji kuwa waangalifu wanapotumia ChatGPT katika juu ya habari zao binafsi. Kwa mfano, kuifanya ijue kalenda yako au kuratibu maandalizi ya chakula.