Dodoma. Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, imepanga kuanzisha mfuko wa ruzuku kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuyasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa fedha za kuendeshea miradi yao.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Agosti 13,2025 na Waziri wa mwenye dhamana, Dk Doroth Gwajima wakati akizungumza katika wiki ya kongamano la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali jijini Dodoma.
Dk Gwajima amesema, lengo la mfuko huo ni kuyasaidia mashirika kuepuka changamoto ya ukosefu wa fedha inayosababishwa na kusitishwa kwa utoaji wa mikopo kutoka kwa wafadhili.
“Hii ni njia ya kuondokana na mikopo inayotokana na masharti magumu na ukosefu wa mikopo kutoka kwa wafadhili tuliokuwa tukiwategemea,” amesema Dk Gwajima.
Amesema tangu Januari mwaka huu kumeshuhudiwa kuwepo kwa mabadiliko ya sera katika maeneo mengi ulimwenguni, jambo hili linachangiwa na utawala mpya wa serikali ya Marekani ambaye alikuwa mfadhili mkubwa wa mashirika hayo.
Amesema ni lazima Serikali kwa kushirikiana na wadau ichukue hatua ili kunusuru jamii za Kitanzania kukumbana na athari mbalimbali.
Katika hatua nyingine ameyataka mashirika hayo kufanya kazi kwa uwazi ili kudumisha misingi ya utawala bora na kutoa nafasi kwa Serikali kuongeza ushirikiano na sekta hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya serikali NaCoNGO, Jasper Makala amesema licha ya mashirika hayo kujitahidi katika kuzisaidia jamii yanakumbana na changamoto za malimbikizo ya kodi, yanayochangia na kutozwa kiasi kikubwa kisicholingana na kiwango cha shughuli na rasilimali za mashirika hayo. Hivyo kushindwa kutekeleza miradi.