Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza fursa za ajira kwa wataalamu wa kada mbalimbali huku wale wenye taaluma ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), wakihitajika zaidi ya wengine.
Kwa mujibu wa tovuti ya sekretarieti ya ajira leo Jumatano Agosti 13, 2025, jumla ya wataalamu 219 wanahitajika kutoka kada 31, kati yao wa Tehama ni 25.
Katika mchanganuo wa mahitaji yao, kama ilivyoainishwa kwenye tovuti hiyo, kada ya uhasibu ina fursa 11, benki, uchumi na huduma za kifedha 13 na sayansi ya maumbile na asilia watatu.
Kwa upande wa kada ya ubunifu na sanaa za uchoraji anahitajika mmoja, wahandisi wa kompyuta na umeme wawili, elimu na mafunzo 13, uhandisi na ujenzi 22 na sayansi ya mazingira na jiografia wanne.
Sambamba na kada hizo, pia kuna fursa za wataalamu 14 wa kilimo na mifugo, sita wa afya na dawa, 24 wa rasilimali watu na utawala, mmoja wa mahusiano ya kimataifa na watatu wa sheria.
Wataalamu wa kada ya isimu au lugha anahitajika mmoja, masoko, vyombo vya habari na uendelezaji wa nembo 14, ununuzi na usimamizi wa ugavi mmoja na usimamizi wa miradi, mipango na sera anahitajika mmoja.
Wengine ni wataalamu wa masomo ya dini mmoja, watafiti, sayansi na bioteknolojia watatu, usalama mmoja, sosiolojia, sayansi ya siasa, jamii na maendeleo ya kijamii watano na takwimu na hisabati watano.
Kwa upande wa wataalamu wa ushuru na hifadhi ya jamii wawili, utalii na usafiri watatu, fundi na huduma mbalimbali wanne, usafirishaji na usafiri wa mizigo saba, madereva tisa, usimamizi wa ardhi wanne, maji, madini na rasilimali asilia 12 na kilimo na rasilimali asilia wanne.