Simba yampandisha ndege beki mpya

‘NA Uanze’ ndivyo unavyoweza kusema kwani Simba inaonekana kupania kufanya mambo mapema tu mara tu baada ya msimu mpya kuanza, baada ya kupiga kambo ya maana kule Ismailia, Misri, huku mastaa wa maana tu wakiendelea kutua hukohuko ili kuzoweana na wenzao.

Hata hivyo, maisha yanaendelea kuwa matamu kwa mastaa hao na kinachoelezwa ni kwamba kuna muunganiko unatengenezwa kambini baina ya mastaa wapya na wale wa zamani ili kipyenga cha kuanza kwa Ligi Kuu Bara na mashindano ya CAF kitakapopulizwa mwezi ujao Wekundu wa Msimbazi wacheke tu.

Lakini, Simba buana wajanja sana. Ikiwa inaingia wiki ya pili sasa kambini huko Misri imempandisha ndege beki wa kushoto wa zamani wa Coastal Union na Singida Black Stars ili kupiga tizi na wenzake wanaojiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa pambano kupelekewa kambini na kuanza kujifua na wenzake, bado hatma ya beki huyo kupewa mkataba ipo mikononi mwa kocha Fadlu Davids anayeendelea kumsoma kabla ya kufanya maamuzi yatakayokuwa na manufaa ya kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Bara.

Inadaiwa mabosi wa Simba, walipokea maelekezo kutoka benchi la ufundi chini ya Fadlu kwamba wanamhitaji, Mkongomani Hernest Malonga aliyemaliza mkataba na Singida Black Stars apelekwe kambini Misri ili wamsome vizuri kabla ya kumpa mkataba. Na kweli beki huyo aliyezitumikia Tabora United na Coastal Union wa mkopo katika mkataba wa miaka miwili aliokuwa nao na Singida akatua huko fasta.

Mwanaspoti imepenyezewa kuwa, Malonga ana siku kadhaa katika kambi ya Simba akifanyiwa majaribio ya Fadlu ili kucheki kama kiwango chake kitamshawishi kumvuta ndani ya kikosi hicho.

Simba ilimpandisha ndege baada ya kubaini ameshamaliza mkataba aliokuwa na Singida na kuwa huru, ili kuona kama anaweza kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Valentin Nouma baada ya Anthony Mligo kuziba ile ya aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyetua Yanga kwa mkataba wa miaka miwili wenye dau nono.

Kutokana na kuwa mchezaji huru, benchi la ufundi na mabosi wa Simba wanaona itakuwa rahisi kwao kumbeba kwani hakutakuwa na fedha za kumnunua, lakini Malonga anaijua vyema Ligi Kuu na ameonyesha kiwango kizuri katika timu zote alizozitumikia katika ligi hiyo tangu alipotua nchini.

Mwanapoti inafahamu kuwa, beki huyo aliyekuwa ameondoka kwenda kwao Kongo – Brazzaville baada ya kumalizika kwa ligi  msimu uliopita, lakini ameitwa na Simba ili kocha Fadlu aweze kucheki kiwango chake kabla ya uamuzi wa kumsajili kutolewa.

Wiki moja iliyopita Mkongomani huyo alitua jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza safari ya kwenda Misri, ili kujiunga na wachezaji wengine waliyoko huko kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Taarifa za ndani zinasema kuwa hatma ya beki huyo bado iko mikononi mwa Simba kama kiwango chake kitamridhisha Fadlu, basi atapewa mkataba.

“Kwa sasa usajili unafanyika kupitia kocha, lazima amuone ubora wake ndio ampitishe na kupewa mkataba, hiyo ndio mipango iliyopo ndio maana wapo waliokuja na kuondoka hukuhuku,” kimesema chanzo hicho kilichodokeza awali kulikuwa na beki Mcameroon Joseph Jonathan Ngwem, lakini alishindwa kulivutia benchi na kukaushiwa ndipo jina la Malonga likafika mezani mwa mabosi.

“Na waliopo kambini haimaanishi wako salama, bado mchujo unaendelea hivyo, kikosi kinaendelea kusukwa kutokana na mashindano watakayocheza msimu ujao, mipango ni kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa.”

Kama Malonga atapita kwenye mtihani huo na kupewa mkataba, basi Simba inabidi ipunguze mchezaji mmoja wa kigeni, kwani tayari imekwisha kufikisha idadi inayotakiwa kusheria kwa wageni (12).

Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa Simba inahesabu kali baada ya kutoka Misri, kwani itawauza na kuwatoa kwa mkopo baadhi ya wachezaji ambao wapo kambini, akiwamo Steven Mukwala, Joshua Mutale na Leonel Ateba wanaodaiwa kuna ofa mezani mwa mabosi wa Simba wanaozijadili.

Mastaa wa kigeni waliyopo Simba kwa sasa ni pamoja na Jonathan Sowah, Jean Charles Ahoua, Alassane Kante, Mohamed Bajaber, Moussa Camara, Steven Mukwala, Neo Maema, Ellie Mpanzu, Joshua Mutale, Leonel Ateba, Rushine De Reuck na Chamou Karaboue.