NAHODHA wa timu ya wachezaji wa ndani ya Nigeria, Junior Nduka ameshindwa kujizuia na kungua kilio baada ya timu yake kutolewa mapema kwenye michuano ya fainali za CHAN kufuatia kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Sudan.
Mechi hiyo ya kundi D ilipigwa juzi, Jumanne ya Agosti 12, 2025 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Dakika chache baada ya kipenga cha mwisho, Nduka alionekana akiketi katikati ya uwanja huku akifunika uso wake kwa mikono, akibubujikwa na machozi.
Wachezaji wenzake walijaribu kumbembeleza, lakini nahodha huyo alishindwa kuzuia hisia zake. Nigeria kwenye mechi hiyo, walionekana kukosa mwelekeo tangu dakika za mwanzo.
Sudan walipata bao la kwanza dakika ya 25 baada ya beki wa Nigeria, Ngenge, kujifunga, kabla ya Walieldin Khidir kuongeza bao la pili kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 44.
Kipindi cha pili kilikuwa cha majonzi zaidi kwa Nigeria, baada ya Tabanja kufunga mabao mawili dakika ya 55 na 62, na kuifanya Sudan kuondoka na ushindi wa mabao 4-0.
Matokeo hayo yamewaacha Nigeria wakiwa hawana pointi baada ya mechi mbili, na hivyo kutupwa nje rasmi ya mashindano.
Nduka, ambaye ni mmoja wa wachezaji wenye uzoefu kwenye kikosi hiki, alisema baada ya mchezo kuwa wamepoteza fursa kubwa ya kuonesha uwezo wao.
“Tulijiandaa, lakini tulifanya makosa ya msingi. Kama nahodha, najihisi nimewaangusha wachezaji wenzangu na nchi yangu,” alisema.