Tano tayari, hao Tausi wabayaa

LIGI ya kikapu Dar es Salaam inaendelea kunoga huku timu zilizotinga hatua ya robo fainali zikianza kujulikana na unaambiwa mambo ya kubaniana ‘press’ kwa timu kwa timu, ubora na yale maokoto ya nje ya uwanja yalitawala msimu huu hadi sasa.

Ligi ya msimu huu inatajwa ni bora zaidi na hadi sasa tayari timu tano zimeshatinga robo fainali ambazo ni Dar City iliyokusanya pointi 30, JKT 26, Pazi 24, Stein Warriors 24 na ABC 23.

Pia kuna timu ambazo bado zinapambana kusaka tatu kutinga hatua hiyo kuungana na zilizotangulia ambazo ni Vijana ‘City Bulls’ yenye pointi 21, Srelio 21, DB Oratory 21, Savio 21 na UDSM 21 na zitamaliza michezo yao ya 15, Jumapili, Agosti 17.

DB Oratory ndiyo timu pekee iliyomaliza michezo 15, huku Srelio ikabakiza  mmoja sawa na Vijana, Savio, Mchenga Star, UDSM na Vijana.

Chui yenye pointi 20, KIUT 19 zenyewe zitasubiri kucheza tena Ligi ya BDL mwakani, huku Kurasini Heat yenye pointi 18 na Mchenga Star 18 zinapambana zisishuke daraja. Mchenga itamaliza na Savio, huku Kurasini Heat ikicheza na Pazi.

Kwa upande zilizoshuka daraja ni Polisi iliyomaliza na pointi 17 na Mgulani JKT 14, timu tatu ndizo zitakazoshuka.

TAN 01

KUPIGANA PINI ‘PRESS’

Unaambiwa huu ni mtego na usipokaa vizuri unapigwa pointi za harakaharaka na mpinzani wako.

Ni hivi. Mbinu hii ni ya kumpana mpinzani katika eneo lake ili kumfunga haraka kama ilivyotokea katika mchezo wa wanawake na Tausi Royals ilicheza dhidi ya Mgulani Stars na mchezo wa JKT Stars na City Queens.

Tausi Royals iliibana Mgulani dakika tatu za mwisho za robo ya nne eneo lake, hali iliyofanya ipate pointi 20 za haraka haraka na kazi hiyo ilifanywa na Tumaini Ndosi, Juliana Sambwe, Diana Mwendi na Tukusubira Mwalusamba na kuifanya Tausi inayoshiriki Ligi ya WBDL kwa mwaka wa pili, kuishinda Mgulani Stars kwa pointi 107-38.    

Katika mchezo mwingine JKT Stars iliishinda City Queens kwa pointi 120 -34, JKT Stars iliibana City Queens dakika mbili za robo ya tatu ya mwisho  ikafunga pointi 25 za haraka haraka.

TAN 03

Katika ligi hiyo, moja ya timu zilizoonyesha ubora ni Dar City baada ya kumaliza michezo yake 15 bila kupoteza ikibeba pointi 30.

Moja ya sababu za ubora wa timu hiyo inatajwa ni usajili uliofanywa na mwekezaji Mtanzania, Mussa Mzenji na ameshusha majina makubwa kutoka ndani na nje ya nchi.

Nyota hao ni Sharom Ikedigwe, Clinton Best (Nigeria), Jamel Marbuary (Marekani) na Victor Mwoka (Kenya), upande wachezaji wazawa ni Amin Mkosa aliyetokea Mchenga Star.

Pia maandalizi mazuri ya timu hiyo, ikiwemo ya usafiri wa pamoja unaowafanya wachezaji kuwa na hali nzuri kwani baadhi ya timu wachezaji hufika uwanjani mmoja mmoja.

Benchi zuri la ufundi pia inatajwa kuchangia timu hiyo kufanya vizuri likiongozwa na kocha mkuu, Mohamed Mbwana akisaidiana na Isiaka Masoud.