Unguja. Baada ya wananchi wa vijiji mbalimbali kisiwani hapa kushuhudia umeme ukipita juu ya nyumba zao bila wao kufikiwa na huduma hiyo kwa muda mrefu, Serikali ya Zanzibar sasa imekuja na sera madhubuti ya kuhakikisha kila kijiji kinaunganishwa na umeme, bila kujali idadi ya wakazi au uwezo wao wa kiuchumi.
Katika kutekeleza sera hiyo, Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) limefanikiwa kuunganisha jumla ya vijiji 186 ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Hatua hiyo imetajwa na wananchi wa maeneo husika kuwa mkombozi mkubwa, si tu kwa kuwaondolea maisha ya giza, bali pia kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 13, 2025, Meneja Mkuu wa Zeco, Haji Haji amesema wakati Rais Hussein Mwinyi anaingia madarakani mwaka 2020, kulikuwa na changamoto nyingi za umeme kwani ulikuwa haujapewa kipaumbele katika maendeleo ya kijamii.
“Kumekuwapo na kasi kubwa ya kupeleka umeme vijijini ambapo kwa kipindi kifupi zaidi ya vijiji 186 vimeunganishiwa kati ya hivyo 36 vipo Pemba katika mazingira ya kawaida hawakufikiria kama wanaweza kupata umeme,” amesema Haji.
Katika hilo, pia Zeco inatengeneza sera kuhakikisha vijiji hivyo pia vinawekewa umeme jua ili kuwapatia fursa wananchi ambao watashindwa kumudu gharama za kuunganishiwa umeme.
“Kazi inaendelea kwa kasi kubwa kuunganisha vijiji vingi, tunataka kuhakikisha wananchi zaidi ya asilimia 80 wanapa umeme kwani Rais Mwinyi ameweka mazingira upatikanaji wa nishati hiyo kwa bei nafuu,” amesema na kuongeza;
“Sera yetu ya sasa popote ambapo laini ya umeme umepita, lazima kuwepo na umeme hakuna kuvuka kijiji wakati zamani nguzo zilikuwa zikipita katikati ya vijiji, lakini unakuta hakuna umeme, zaidi ya miaka 40 umeme umepita juu wananchi wakishuhudia tu,” amesema.
Meneja huyo amesema katika mradi wa Benki ya Dunia (WB) ambao unatarajia kuanza kutekelezwa mwaka 2027, kuna kipengele maalumu ambacho kinataka kaya maskini 70,000 ziunganishiwe umeme kwa gharama nafuu na zitafidiwa na mradi, huku mradi wa Benki ya Maendeleo Afrika ukitarajia kuunganisha kaya maskini 30,000.
Badru Haji Khamis mkazi wa Kijiji cha Makontena Jumbi amesema walikuwa wanaadhirika na tatizo la umeme, lakini kwa sasa wanafurahia maisha,” amesema Khamis.
Mwananchi mwingine wa Kijiji cha Nyakurungu, Mohamed Othmn Mbarouk amesema, “tunashukuru sasa tunafanya biashara.”
Sharifa Ahmada Haji mkazi wa Kijiji cha Mkorogo, amesema umeme umepunguza hata matukio ya uhalifu ambayo yalikuwa yakitokea kwenye maeneo yao kutokana na kuwapo kwa giza.
Meneja huyo amefafanua kuwa kabla ya mwaka 2025, mtu alipokuwa akitaka kuunganishiwa umeme kwa mita ya ‘phase’ moja, alipaswa kulipa Sh464,000 lakini kwa sasa imepunguzwa hadi kufikia Sh200,000 bila kujali unahitaji nguzo au vifaa vingine.
Kwa upande wa mita ya ‘phase’ tatu ilikuwa Sh886,000 imepungua hadi Sh402,500,
Amesema kutokana na punguzo hilo kumekuwapo na ongezeko kubwa la wananchi wanaotaka kuunganishiwa umeme na idadi yao imepanda kutoka 15,426 na kufikia 105, 824 wastani wa waombaji wapya 32,166 kila mwaka ikiwa ni ongezeko la asilimia 103.