Wananchi 103 wa maeneo yaliyotwaliwa Dodoma walipwa mamilioni

Dodoma. Serikali kupitia Wizara ya Maji, imekamilisha ulipaji fidia yenye jumla ya Sh999 milioni kwa wananchi 103 wa maeneo yalitwaliwa yakiwamo Nzuguni, Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa jijini Dodoma.

Lengo ni ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa).

Ulipaji wa fidia hizo, umeongozwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Duwasa, Wizara ya Ardhi na viongozi wa serikali za mitaa ya maeneo husika.

Mchanganuo ulivyo kwa eneo la Nzuguni, wananchi 24 wamelipwa fidia ya Sh148 milioni, Agosti 7, 2025, Zuzu Nala wananchi 51 wamelipwa fidia ya Sh594 milioni, Agosti 11, 2025, Nala Chihoni wananchi saba walilipwa fidia yao ya Sh58 milioni tangu Aprili, 2025.

Aidha, Kibaigwa wananchi 23 wamelipwa fidia ya Sh197 milioni na kukamilisha hatua hiyo Agosti 12, 2025.

Akizungumza jana Jumanne, Agosti 12, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Aron Joseph ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa wananchi waliotoa ardhi yao kupisha utekelezaji wa miradi ya maji.

“Duwasa, kwa niaba ya wananchi wa maeneo haya naishukuru Serikali ya awamu ya sita na Wizara ya Maji kwa juhudi zao kubwa na ufanisi katika kuhakikisha ulipaji wa fidia kwa wakati kwa wananchi wetu.

“Hatua hii ni muhimu kwa maeneo yaliyotekelezwa na yanayoendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya kimkakati katika Jiji la Dodoma na Kanda ya Kibaigwa, hii inaonesha dhamira ya Serikali katika kulinda haki za wananchi wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesema Aron.

Kwa upande wake, Josephina Paulo ambaye ni mkazi wa Kibaigwa ameishukuru Serikali kwa kuwasikiliza na kuwalipa fidia. Ameiomba kwa kuwaona wanyonge na kuwafikia wengine ambao bado hawajalipwa wanasubiri kulipwa.

Naye, Yohana Mwarabu ameshukuru Serikali kwa kumjali na kumlipa kwani sasa atakwenda kujenga nyumba nyingine ili aweze kuishi na familia yake ambapo awali hakuwa na matumaini lakini kwa sasa ana amani.

Fidia hiyo ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na Serikali kupitia Duwasa iliyokusudiwa kuboresha upatikanaji wa majisafi na huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa jiji la Dodoma na maeneo mengine yanayohudumiwa na mamlaka hiyo.