Watu 25 Wafukiwa na Kifusi Shughuli za Ukarabati Mgodi Shinyanga – Video – Global Publishers



Watu 25 wamefukiwa na kifusi katika mgodi mdogo wa dhahabu unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi, uliopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, baada ya mgodi huo kutitia wakati wa zoezi la ukarabati wa maduara.

 

Tukio hilo limetokea majira ya asubuhi ya Agosti 11, 2025, ambapo wahanga walikuwa wakifanya matengenezo katika mashimo matatu tofauti:

Duara namba 106 — watu 6

Duara namba 103 — watu 11

Duara namba 20 — watu 8

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa wa Shinyanga imefika eneo la tukio kutoa pole na kushiriki katika zoezi la uokoaji, likiwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wachimbaji wa mgodi huo.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kutitia kwa ardhi wakati shughuli za ukarabati zikiendelea. Hadi sasa, watu saba kati ya 25 wameokolewa wakiwa hai, huku jitihada za kuwaokoa waliobaki zikiendelea kwa nguvu zote.