Yanga yaipiga bao tena Simba

Simba na Yanga buana! Timu hizo zenye mashabiki wengi nchini zimeendeleza bato ambalo aslani wana Msimbazi wasingependa kuliona au kulisikia.

Wababe hao wa Ligi Kuu Bara hivi sasa wanapambana kuweka sawa vikosi ili wakaliamshe katika mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.

Lakini, wakati hilo likiendelea Shirikisho  la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS), limetoa orodha ya klabu 20 bora Afrika, ambapo Yanga imeendelea kufanya vizuri kutokana na mafanikio mbele ya wapinzani na watani zao hao wa jadi nchini.

Yanga ambao ni mabingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara katika orodha hiyo inashika nafasi ya tisa Afrika na 182 duniani, huku Simba ikishika ya 10 Afrika na ya 185 duniani.

Katika orodha hiyo Pyramids ya Misri inashika nafasi ya kwanza Afrika na 50 duniani, huku Al Ahly kutoka Misri pia ikiwa ya pili na 65 duniani, wakati RS Berkane ya Morocco iko nafasi ya tatu Afrika na ya 85 duniani.

Zamalek ya Misri inashika nafasi ya nne Afrika na 104 duniani, Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia iko nafasi ya tano Afrika na 115 duniani, wakati Mamelodi Sundowns FC ya Afrika Kusini ya sita Afrika na 124  duniani.

Orlando Pirates FC ya Afrika Kusini inashika nafasi ya saba Afrika na ya 158 duniani  wakati FAR Rabat ya Morocco ni ya nane na ya 172 duniani, huku Yanga ikishika nafasi tisa ikifuatiwa na Simba inayohitimisha 10 bora kwa ubora Afrika.

Al Masry ya Misri inashika nafasi ya 11 Afrika na ya 203 duniani ikifuatiwa na MC Alger ya Algeria inayoshika nafasi ya 12 Afrika na 214 duniani, huku CR Belouizdad ya Algeria  ikishika ya 13 Afrika na ya 218 duniani.

USM Alger iko nafasi ya 14 Afrika kwa ubora ikifuatiwa na CS Constantine ya Algeria pia iliyo nafasi ya 15, huku zote zikiwa nafasi ya 231 duniani ilhali Raja Casablanca ya Morocco ikiwa nafasi ya 16 Afrika na 241  duniani.

Stellenbosc ya Afrika Kusini inashika nafasi ya 17 Afrika na 295 duniani ikifuatiwa na Al Hilal Omdurman ya Sudan inayoshika ya 18 Afrika na 304 duniani, huku US Monastir ya Tunisia ikiwa ya 19 Afrika na ya 393 duniani.

Timu ya mwisho katika 20 bora za ubora wa viwango Barani Afrika ni AS Maniema Union ya DR Congo ambapo kwa duniani inashika ya 393 sambamba na ile ya US Monastir ya Tunisia, ingawa mara ya mwisho ilishika nafasi ya 380 duniani.