TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imefungua rasmi mafunzo ya siku saba kwa Maafisa Wasimamizi Wasaidizi wa majimbo yote 50 ya uchaguzi kama sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utakaofanyika Oktoba 2025.
Akizungumza katika ufunguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Mhe. Jaji Aziza Iddi Suwedi, amepongeza maafisa hao kwa kuteuliwa kushika majukumu hayo nyeti na amewataka kutambua kuwa wana dhamana kubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi.
“Mnakwenda kuwa wawakilishi wa Tume kwenye majimbo yenu, mkiwa na jukumu la kuongoza maandalizi, utekelezaji na ufuatiliaji wa uchaguzi katika ngazi ya jimbo. Nidhamu, uadilifu, usiri wa kazi na utiifu kwa taratibu za Tume lazima viwe nguzo zenu kuu,” amesema.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 34 cha Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018, Tume inawajibika kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kila baada ya miaka mitano, na kwamba ifikapo Oktoba mwaka huu Zanzibar itaendesha uchaguzi wa saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Amefafanua kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuvunjwa rasmi kwa Baraza la Wawakilishi tarehe 13 Agosti 2025, na kwamba Tume inatarajia kutangaza tarehe ya uteuzi wa wagombea na uchaguzi ifikapo tarehe 18 Agosti mwaka huu.
Jaji Aziza ameutaja uchaguzi huo kama fursa muhimu ya kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na amani, na amewataka maafisa hao kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria, haki na kwa uwazi ili wananchi waamini mchakato huo.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanahusisha mada 15, ikiwemo sheria na kanuni za uchaguzi, uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura, majumuisho, usimamizi wa fedha na ushiriki wa makundi maalumu.
“Ninatarajia mshirikiane kwa karibu na wadau wote wa uchaguzi kupitia mawasiliano ya wazi, ushirikiano na uwajibikaji. Mafanikio ya uchaguzi huu yanategemea sana utendaji kazi wenu,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Thabit Idarous Faina, amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018, kutaendelea kuwepo na kura ya mapema kwa baadhi ya makundi maalumu.
Amesema kura hiyo inalenga kuhakikisha kwamba wale ambao hawawezi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa sababu za kikazi au mazingira maalumu wanapata nafasi ya kutumia haki yao ya kikatiba mapema.
“Ni wajibu wa Tume kuhakikisha kila mpiga kura anapata fursa ya kushiriki bila vizuizi. Hivyo, kura ya mapema ni njia ya kujumuisha wote,” amesema Faina.
Amewataja walengwa wa kura ya mapema ni pamoja na maafisa wa uchaguzi na wasaidizi wao watakaokuwa na majukumu siku ya uchaguzi, maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama watakaokuwa kazini, wahudumu wa afya watakaokuwa zamu,na watu wengine waliooanishwa kwenye sheria hiyo.