Ajira Tanzania kipimo kipya cha ahadi za CCM katika ilani

Katika historia ya siasa za uchaguzi nchini Tanzania, ilani za Chama cha Mapinduzi (CCM) zimekuwa zikiakisi matarajio ya kisera ya chama hicho katika kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030 imeweka alama ya kipekee kwa kulipa uzito mkubwa suala la ajira, ambapo neno ‘ajira’ limetajwa mara 82, ishara ya dhahiri kwamba upatikanaji wa ajira si suala la kisiasa tu, bali pia ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa Taifa.

Katika uchambuzi huu, tunaangazia kwa kina jinsi CCM ilivyokusudia, na kwa kiasi gani imefanikiwa, kutekeleza upatikanaji wa ajira, pamoja na changamoto na maeneo yanayohitaji msukumo zaidi kuelekea mwaka 2030.

Takwimu zilizowasilishwa katika ilani hiyo zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2020 hadi 2024, Tanzania ilisajili miradi 901 ya uwekezaji kupitia TIC yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 9.31, ikilinganishwa na miradi 207 yenye thamani ya Dola milioni 1.09 mwaka 2020.

Miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira 212,293. Hii ni dalili kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yameimarishwa kwa kiwango kikubwa, na hatua hii imechangia kwa namna moja kwa moja kuongeza ajira, hasa kwa vijana.

Ingawa takwimu hizi zinaonesha mafanikio makubwa, ni muhimu kutazama pia ubora wa ajira hizo, je, ni ajira za muda mrefu, zenye staha na zinazoendana na viwango vya kazi vinavyokubalika kitaifa na kimataifa?

Kwa mujibu wa ilani hiyo hiyo, ajira zipatazo 8,084,203 zilitengenezwa katika sekta rasmi na isiyo rasmi ndani ya kipindi hicho, ambapo sekta isiyo rasmi ilichangia ajira 7,037,024 na sekta rasmi 1,047,179 pekee

Hii ina maana kuwa zaidi ya asilimia 87 ya ajira zilizozalishwa zilikuwa katika sekta isiyo rasmi, hali inayozua hoja kuhusu usalama wa ajira hizo, hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi, pamoja na uhakika wa kipato.

Ajira zisizo rasmi mara nyingi hukosa mikataba ya kazi, pensheni, huduma za afya na usalama wa kazi. Hili linaweka mzigo kwa Serikali baadaye katika kulinda ustawi wa wafanyakazi.

Pamoja na hayo, Serikali imefanikiwa kutumia sekta za kimkakati kama kilimo, viwanda, utalii, nishati na ujenzi kuendesha ajenda ya ajira.

Kwa mfano, katika sekta ya kilimo, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 18.6 mwaka 2020 hadi tani milioni 22.8 mwaka 2024, na matumizi ya mbolea yakiongezeka kwa asilimia 107.

Vilevile, maeneo ya kilimo cha umwagiliaji yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 80.

Kwa ujumla, maboresho haya katika sekta ya kilimo si tu yameongeza usalama wa chakula, bali pia yamefungua nafasi nyingi za ajira, hasa vijijini, katika uzalishaji, usindikaji na usambazaji wa mazao.

Sekta ya viwanda imepewa msukumo mkubwa, ambapo zaidi ya viwanda 47,063 vimeanzishwa, kati yake viwanda vikubwa ni 365, vya kati 1,360 na vidogo 45,338.

Hii imesaidia kuchochea ajira na kuongeza mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi kutoka Dola milioni 908.6 hadi Dola milioni 1,363.3 kufikia mwaka 2024.

Kwa mantiki hiyo, mkakati wa kujenga viwanda kwa kila mkoa na wilaya, kama ilivyopendekezwa katika ilani, unaonekana kuwa na mantiki ya kuendeleza ajira kwa kuhusisha moja kwa moja thamani ya mazao ya kilimo, misitu, uvuvi, madini na bidhaa za ujenzi.

Katika sekta ya utalii, kwa mujibu wa ilani hiyo, idadi ya watalii wa nje iliongezeka kutoka 620,867 mwaka 2020 hadi zaidi ya milioni 2 mwaka 2024, na mapato kutoka Dola milioni 700 hadi Dola bilioni 4.

Kwa kawaida, sekta hii hutoa ajira kwa maelfu ya watu, kuanzia kwa waongozaji wa watalii, wapishi, wahudumu wa hoteli, hadi kwa wachuuzi wa bidhaa za utamaduni.

Ilani imepanga kuongeza ajira kwenye sekta hiyo kutoka milioni 1.5 mwaka 2024 hadi milioni tatu ifikapo mwaka 2030.

Changamoto iliyopo ni kuhakikisha kuwa ongezeko hilo la ajira linakwenda sambamba na mafunzo ya kitaalamu ili kuimarisha viwango vya huduma na ushindani wa kiuweledi.

Vilevile, zaidi ya Sh3.69 trilioni zilitolewa kama kandarasi kwenye mradi wa SGR, ambao unatajwa kuzalisha zaidi ya ajira 180,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Hii inaonesha namna miradi mikubwa ya kimkakati inavyoweza kuwa kichocheo cha ajira.

Katika upande wa Zanzibar, takwimu zinaonesha kuwa ajira 217,500 zimetengenezwa, ikiwa ni asilimia 72.5 ya lengo la ajira 300,000 kufikia mwaka 2025.

Zanzibar inalenga kuzalisha ajira mpya 350,000 kufikia mwaka 2030. Hii inaonesha msimamo wa pande zote mbili za Muungano katika kulipa kipaumbele suala la ajira, hasa kwa vijana.

Kwa upande mwingine, ilani imeonesha dhamira ya kuanzisha vituo vya kukuza stadi kwa vijana, programu za kuhamasisha ajira nje ya nchi, na kupitia upya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Hatua hizi, kwa pamoja, zikitekelezwa ipasavyo, zinaweza kuibua nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa na kubadilisha muundo wa ajira nchini kutoka ule wa kutegemea sekta zisizo rasmi kwenda kwenye sekta zenye tija, rasmi na zenye mchango mkubwa kwa uchumi.

Hata hivyo, ipo changamoto kubwa ya kutokuwapo kwa usawa wa kijiografia katika kuanzisha ajira.

Ajira nyingi zinapatikana zaidi katika mikoa ya mijini na maeneo yaliyo karibu na fursa za kiuchumi kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

Ili kuhakikisha upatikanaji wa ajira unakuwa jumuishi, Serikali inapaswa kuharakisha uwekezaji katika miundombinu ya kijamii na kiuchumi katika mikoa ya pembezoni.

Vilevile, ajira katika sekta rasmi zinapaswa kuongezeka kwa kasi. Ilani ya CCM inalenga kwamba angalau asilimia 50 ya ajira milioni 8 zinazolengwa katika miaka mitano ijayo ziwe katika sekta rasmi.

Ili kufikia lengo hilo, ni lazima kuharakisha urasimishaji wa ajira katika sekta isiyo rasmi, kupitia usajili wa kampuni ndogo, kutoa elimu ya kifedha, na kuhakikisha wajasiriamali wanapata mikopo na mitaji kwa masharti nafuu.

Kwa kuhitimisha, Ilani ya CCM ya 2020–2025 imetoa mwelekeo mahususi wa kukuza ajira, na utekelezaji wake hadi mwaka 2024 unaonesha mafanikio ya takwimu, hususan kwenye uzalishaji wa ajira, ufadhili kwa makundi maalumu na ujenzi wa sekta za kimageuzi.

Hata hivyo, kuna haja kubwa ya kuongeza ubora wa ajira, kuzifanya rasmi, kuhimiza ujuzi unaohitajika kwenye soko la sasa, pamoja na kuhakikisha usawa wa fursa kwa makundi yote ya kijamii.

Kadiri Taifa linavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, ajira itabaki kuwa kipimo kikuu cha namna ahadi za kisiasa zinavyoakisi hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida.