Hai. Askari wanafunzi 10 kati ya 14 wa Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi, mkoani Kilimanjaro waliopata ajali ya gari wameruhusiwa kuendelea na matibabu katika hospitali ya Polisi iliyopo shuleni hapo baada ya afya zao kuimarika.
Wanafunzi (kuruta) wengine wanne wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, mkoani hapa huku mmoja aliyepata rufaa akiendelea na matibabu katika hospitali ya KCMC baada ya kuvunjika mbavu tatu.
Ajali hiyo ilitokea jana, Agosti 12, 2025 eneo la Kwasadala, Wilayani Hai na kujeruhi askari wanafunzi 15 baada ya gari lililobeba wanafunzi hao likitokea kambi ya polisi iliyopo wilayani Siha kugongana uso kwa uso na gari aina ya fuso iliyokuwa ikitokea Wilaya ya Moshi kwenda wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Agosti 13, 2025, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Emmanuel Minja amesema wanafunzi hao wanaendelea vizuri na kusema 14 waliosalia jana katika hospitali hiyo baada ya mmoja kupewa rufaa Hospitali ya KCMC, 10 wamepelekwa hospitali ya shule hiyo kuendelea na matibabu.
“Wanaendelea vizuri, tumebakia na wanafunzi wanne wengine tuliwaruhusu waendelee na huduma hospitali ya jeshi (TPS),” amesema Dk Minja.
Awali, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu alitoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.
“Nieendelee kutoa wito kwa madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani, kwani mkoa wetu haujatulia na hizi ajali zinatokea mara kwa mara,”amesema RC Babu.
Ajali hiyo ilitokea ikiwa zimepita siku 15 tangu kutokea kwa ajali iliyosababisha vifo vya watawa wawili wa Kanisa Katoliki na majeruhi 11 eneo la Bomang’ombe Wilayani humo.