Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia askari wanne wa Jeshi la Uhifadhi (Jeshi Usu) kwa tuhuma za mauaji ya kijana mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Eziboni Fikiri (20), mkazi wa Kijiji cha Msonga, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Mauaji hayo yametokea Agosti 13, 2025 saa 12 asubuhi katika Pori la Hifadhi ya Kigosi lililopo wilayani humo.
Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo Alhamisi Agosti 14, 2025 na kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii ya jeshi hilo, imeeleza kuwa askari hao walikuwa wakiwakamata watu walioingia kwenye hifadhi hiyo na kukata miti kinyume na sheria.
Katika taarifa hiyo, iliyosainiwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro imeeleza mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe.
Amedai watuhumiwa wa mauaji hayo wanashikiliwa kwa uchunguzi huku mwili huo ukisubiri hatua za uchunguzi na utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalowakabili.
Jeshi la Polisi limewaomba wananchi kuwa watulivu wakati wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.