Azam FC yasaka mrithi wa Mustafa

KUNA taarifa zimeelezwa Azam FC ina mpango wa kuachana na kipa wake Mohamed Mustafa aliyemaliza msimu uliyopita akiwa na cleansheets 10 na ipo katika mchakato wa kusaka mbadala wake.

Kwa mara ya kwanza Mustafa alijiunga na Azam Februari 7, 2024 akitokea klabu ya El Mereikh ya Sudan, lakini baada ya kufanya mazoezi chini ya kocha mpya Florent Ibengé, imeonakana kuna uhitaji wa kupata kipa mwingine.

Chanzo cha uhakika wa taarifa hiyo kilisema: “Kocha anahitaji atafutiwe kipa mwingine ndiyo maana alihitaji kuwaona wachezaji wote ili ajue ataendelea na nani na kina nani wataachwa.

“Mambo ya ufundi tumemwachia kocha mwenyewe, maana ndiye anayejua kikosi chake kinatakiwa kiwe na sifa gani, mbali na kipa akitaka kuwaacha wachezaji wengine atasema na sisi tutayafanyia kazi mahitaji yake, kikubwa Azam ifikie malengo yake msimu ujao.”

Miongoni mwa majina yanayotajwa huenda yakawa mbadala wa Mustafa ni Issa Fofana kutoka Al-Hilal Club (Omdurman), amezaliwa Januari 30, 2004 (21).

Chanzo pia kimedai timu hiyo inafuatilia makipa katika mashindano ya CHAN yanayoendelea kwa sasa.