:::::::
Kikao cha Kawaida cha Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambacho ni maandalizi ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kimehitimishwa jijini Antananarivo Agosti 14, 2025.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb).
Mawaziri katika kikao hicho ambacho kilishuhudiwa Madagascar wakipokea uenyekiti kutoka kwa Zimbabwe walipitia na kujadili agenda mbalimbali zinazolenga kukuza na kuimarisha mtangamano wa kikanda, ambao ulielezwa kuwa ndiyo njia pekee ya nchi za SADC kufikia agenda ya maendeleo.
Agenda zilizojadiliwa na Waheshimiwa Mawaziri ni pamoja na hali ya michango ya nchi wanachama; taarifa ya utekelezaji ya Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC, Mhe. Elias Magosi ambayo iliangazia masuala ya kiuchumi, siasa, amani na uslama; utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Mawaziri na maamuzi ya Wakuu wa Nchi na Serikali; hali ya nchi wanachama kuridhia itifaki za SADC na nyenzo nyingine za kisheria na agenda zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Mkutano huo utaendelea Agosti 15, 2025 kwa Mkutano wa Utatu wa Makatibu Wakuu na Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na Agosti 16,2025 kwa Mkutano wa Utatu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Wakuu wa Nchi na Serikali. Ikumbukwe Tanzania ni Mwenyekiti wa mikutano hiyo ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama.