Ceasiaa Queens yabeba kiungo jeshini

BAADA ya kukamilisha usajili wa Wakenya wawili, Ceasiaa Queens inaendelea kushusha vifaa na safari hii imemalizana na kiungo mshambuliaji Halima Mwaigomole kutoka Mashujaa Queens.

Timu hiyo ilimaliza nafasi ya sita msimu uliopita katika mechi 18, ikishinda sita, sare tatu na kupoteza mechi tisa, ikifunga mabao 25 na kuruhusu 37, ikikusanya pointi 21.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka alisema usajili wa kiungo huyo unaweza kuongeza ushindani kwenye kikosi hicho chenye njaa ya kufanya vizuri msimu ujao.

Chobanka aliongeza usajili wa wachezaji msimu huu utazingatia zaidi wachezaji wenye uzoefu wa ligi na mchanganyiko wa mabinti wadogo wanaoanza soka.

“Mimi ni muumini wa kuamini vijana wadogo, msimu huu tunachanganya wale vijana wadogo ili kuwapatia uzoefu na kujiamini na wale wenye uzoefu ambao tunaamini wanaweza kutupatia matokeo,” alisema Chobanka.

“Malengo ni kumaliza nafasi nne za juu, hivyo huwezi kuwa na wachezaji wachanga pekee, utahitaji na wale waliokomaa na hilo nimekuwa nikilifanya tangu nikiwa Alliance, ndiyo maana wakati ule ilizalisha vijana wengi ambao ni tegemeo kwa timu zao.”

Mwaigomole, mbali na kuichezea Mashujaa, alipita timu za Panama Girls, Yanga Princess, Baobab Queens na sasa Ceasiaa Queens.