Dodoma. Takriban watu 137,000 hufa kila mwaka barani Afrika na wengine milioni 91 wakiugua kutokana na kula chakula kisicho salama.
Kutokana na hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na suala la usalama wa chakula limekutana ili kupitia upya sera za usalama wa chakula za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuhakikisha kuwa suala hilo linapewa kipaumbele.
Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Serera amesema suala la usalama wa chakula siyo la kufanyia mzaha.

Naibu katibu mkuu wizara ya viwanda na biashara Dk Suleiman Serera
Dk Serera amesema hayo leo Alhamisi Agosti 14, 2025 kwenye warsha ya kitaifa ya utetezi na usambazaji wa muhtasari wa sera ya usalama wa chakula kwa watunga sera wa ngazi ya juu nchini iliyoandaliwa na Shirika la kilimo na chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Amesema idadi hiyo ya watu wanaougua au kupoteza maisha kutokana na changamoto ya chakula kisicho salama na kwamba huo siyo msiba tu wa kibinadamu, bali pia ni hasara ya kiuchumi inayogharimu mabilioni ya dola kutokana na kupotea kwa tija na fursa za kibiashara.
Dk Serera amesema chakula kisicho salama kinadhoofisha uwezo wa kushindana kimataifa, kinapunguza imani ya walaji na kinatishia ndoto ya mapinduzi ya viwanda hivyo jitihada zinahitajika kulinda Taifa kupitia usalama wa chakula.
“Ile ndoto ya Tanzania kuwa kapu la usalama wa chakula barani Afrika hatuwezi kuifikia kama chakula tunachozalisha siyo salama, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunazalisha chakula salama kwa ajili ya kitaifa, kikanda na kimataifa,” amesema Dk Serera.

Baadhi ya washiriki wa warsha ya kitaifa ya utetezi na usambazaji wa muhtasari wa sera ya usalama wa chakula kwa watunga sera wa ngazi ya juu nchini iliyofanyika leo Agosti 14, 2025 Jijini Dodoma
“Ndiyo maana tunashirikiana na wenzetu wa kimataifa kuhakikisha kwamba tunafanya haya mambo pamoja na kama tukipuuza mapungufu madogo ya leo tutajikuta tunakabiliana na matatizo makubwa kesho na hatuko tayari kwa jambo hilo,”
Ametoa wito kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja haliwezi kuachwa mikononi mwa wizara au taasisi moja hivyo hatua za usalama wa chakula ziingizwe katika sera zote iwe ni kilimo, afya, biashara pamoja na mazingira na kuziwezesha mamlaka za serikali za mitaa kudhibiti viwango katika masoko yote rasmi na yasiyo rasmi kwa sababu wao ndiyo wanaoyasimamia.
“Tusaidie wajasiriamali wadogo na wa kati (SME) kutumia viungo vya chakula kwa usalama kuweka lebo sahihi na kudumisha usafi na tuazimie kuimarisha sauti za walaji ili mahitaji ya chakula salama yawe nguvu ya utekelezaji,” amesema

Baadhi ya washiriki wa warsha ya kitaifa ya utetezi na usambazaji wa muhtasari wa sera ya usalama wa chakula kwa watunga sera wa ngazi ya juu nchini iliyofanyika leo Agosti 14, 2025 Jijini Dodoma
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Ashura Katunzi amesema sera hizo zimeanzishwa ili kuona kama kuna mapungufu yafanyiwe kazi na kuleta uhamasishaji ili kuyatekeleza na kuhakikisha kwamba chakula kinachokuwepo kinakuwa bora na salama.
“Tunaposema chakula ni kile ambacho inazalishwa kutoka mashambani, mifugo na vile vinavyotoka kwenye maziwa, mito na bahari vyote kwa ujumla wake kuhakikisha vinakuwa salama. Kuna vichafuzi vingine vinatokana na mazingira na michakato ya uzalishaji hivi vyote vinatakiwa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha chakula kinakuwa salama,” amesema Dk Katunzi.
Naye Mratibu wa miradi FAO, Diomedes Kalisa amesema wao ni wadau wakuu ambao wanashirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutengeneza viwango vya chakula ambavyo vinasaidia nchi kuangalia usalama wa chakula kinachotumika ndani ya nchi, lakini na kuona namna ya kupanua wigo wa biashara wa hivi vyakula katika masoko ya nje.