TETESI nyingi sana zilitolewa kuhusu kiungo wa soka, Feisal Salum Abdallah ambaye hapa kijiweni na maeneo mengi Tanzania tumezoea kumuita Fei Toto na kule Zanzibar wanamuita Failasufi.
Kuna kipindi watoa tetesi walituaminisha dogo anaondoka pale kwa wauza aiskrimu na kurejea timu aliyoichezea kabla ya kutua Chamazi kwa maana ya Yanga na kila kitu kipo freshi kabisa ameshavuta kibunda cha Jangwani.
Tukaambiwa hadi mama yake kapelekwa kutimiza moja ya nguzo muhimu za dini yake na ameshasemehe kwa yote yaliyotokea hapo nyuma na ametoa baraka zote kwa kijana wake kurejea kwa Wananchi.
Baadaye zikavuma tetesi za Failasufi kutua mitaa ya Msimbazi na tajiri namba moja Afrika, Mohammed Dewji keshafanya yake na kijana amekubali kuvaa jezi nyekundu na nyeupe kwani anataka apate raha za kushabikiwa na umati.
Kumbe bwana wale matajiri kule Azam Complex walikuwa wanawachora tu watoa tetesi na walikuwa wanaandaa kitu kizito cha kuwapiga kichwani kwa kumsainisha mkataba mpya kiungo huyo ambao utamfanya abaki hapo kwa muda mrefu zaidi.
Juzi wakafanya yao kwa kumsainisha dogo mkataba mnono wa mwaka mmoja ambao utamfanya awepo klabuni hapo hadi 2027 ambapo nasikia kavuta zaidi ya Shilingi 500 milioni kama dau la kusajili na atalipwa mshahara mnono.
Sisi hapa Kijiweni tunampa hongera sana Fei Toto kwa uamuzi ambao hatuwezi kusema ni mgumu bali ni mzuri wa kuendelea kubakia Azam ili aendelee kuchota noti za familia ya Mzee Bakhresa.
Fei Toto ameyajali zaidi maisha yake ya baadaye kuliko sifa ya kuchezea timu kubwa ambazo atakapokuja kuachana na soka hazitomsaidia kuendesha maisha yake kama ambavyo kaka zake wengi imewatokea baada ya kutekwa na mashabiki.
Kuna wengi ambao walitoa mchango mkubwa kuzibebesha makombe Yanga na Simba leo hawakumbukwi na wanaishi maisha magumu Iła historia ya mafanikio inabakia kwa klabu.