Dar es Salaam. Mtunzi na mwimbaji wa wimbo wa ‘No reforms no election’, George Mwingira, amefariki dunia akitajwa kuacha pengo na maumivu makbwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na familia yake.
Uongozi wa Chadema umemtaja Mwingira kama kijana aliyekuwa mvumilivu, mpambanaji na asiyekata tamaa katika kutekeleza majukumu yake, wakati familia ya msanii huyo ikisema alikuwa mkarimu na mwenye upendo kwa watu wote.
Msanii huyo aliyefahamika kama ‘MC Mwingira’ ambaye alijizolea umaarufu kwa utunzi wa nyimbo za hamasa za Chadema, akitamba kupitia vibao vya “No reforms no election” na wimbo wa “Tundu Lissu wapeleke mchakamchaka”.
Alifariki dunia Agosti 10, 2025 katika ajali ya basi iliyotokea Mikumi mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Belle Ponera, Mwingira alikuwa akitoka Songea, Mkoa wa Ruvuma kwenda Dar es Salaam kuhudhuria kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Kifo hicho, kimeongeza pigo kwa Chadema baada ya msanii wake huyo wa tatu kufariki dunia, baada ya Fulgence Mapunda ‘Mwanacotide’ aliyewahi kutamba na nyimbo za “Chadema People’s Power” na “Polisi msitupige mabomu, Chadema ni Serikali ijayo.”
Mwanacotide alifariki dunia mwaka 2019, akifuatiwa na Sarah Alex aliyetamba na wimbo wa “Mwamba tuvushe” aliyefariki dunia mwaka 2022.
Heche, familia wamzungumzia
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Agosti 14, 2025, Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesema chama hicho, kimepata pigo kubwa kutokana na kifo cha Mwingira aliyekuwa msanii kiongozi kwa kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali.
“Nimemfahamu Mwingira kwa muda mrefu tangu Mwanacotide (marehemu) akiwepo, amepambana sana hadi hapo alipofikia, haikuwa kazi rahisi kwake. Wakati ule kulikuwa na wasanii, lakini Mwingira alivumilia hadi kutoka na kuwa msanii mkubwa ndani ya Chadema,” amesema.
“Kuna kipindi alikuwa anatunga nyimbo lakini haziwezi kusikika, si unajua kiongozi anaweza kukubania, lakini Mwingira hakukata tamaa au kujaribu kukimbia. Mwingira ametutoka akiwa msanii kiongozi wa chama, tumeumia sana,” amesema Heche.
Wakati Heche akieleza hayo, mmoja wa wanafamilia wa Mwingira aliyeomba jina lisitajwe, amesema ndugu yao alikuwa mtu mwenye unyenyekevu na tegemezi katika familia yao.
“Katika familia yao kina Mwingira wamezaliwa wanne kati yao wakiume wawili. Ameacha mtoto mmoja wa kike, amesema.
“Alikuwa mtu mwenye upendo ndani na nje ya familia, tumepoteza mtu muhimu sana,” amesema mwanafamilia huyo.
Taarifa ya kifo cha Mwingira
Ponera, amesema: “Mwingira alikuwa anasafiri kwenda Dar es Salaam, kuhudhuria kesi ya Lissu, tulikuwa tuna mawasiliano naye mazuri lakini ghafla yalikata.”
“Baada ya kuona kimya ilibidi tuanze kutafuta taarifa ya nini kimetokea, tukaambiwa kuna ajali imetokea lakini wahusika walificha kutoa taarifa. Ndio maana utaona kifo kimetokea Jumapili, taarifa zimepatikana leo,” amesema Ponera.
Kwa mujibu wa Ponera, haikuwa kazi rahisi kujua kilichompata MC Mwingira, lakini baada ya kutuma timu ya watu waliokwenda hadi Mikumi, kisha kutembelea hospitali mbalimbali ndipo wakabaini rafiki yao amefariki dunia.
“Tunasubiri taratibu za kipolisi ili kuuchukua mwili wa Mwingira utakaosafirishwa kwenda Songea kwa ajili ya mazishi. Nimewasiliana na familia ya Mwingira hatutachelewa kumzika mpendwa wetu,” amesema Ponera.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema kwa sasa chama hicho kipo kwenye majadiliano na familia kwa ajili ya taratibu za kuutoa mwili wa Mwingira katika Hospitali ya Misheni Mikumi kwenda Songea mkoani Ruvuma kwa mazishi.
“Tumepata pigo, Mwingira alikuwa msanii mkubwa wa chama na wimbo wake wa mwisho ulikuwa ‘No reforms no election na tulifanya kila jitihada ili kuhakikisha unaimbwa na umma, tutamkumbuka sana,” amesema Rupia.