Na mwandishi Maalumu
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, yupo Cape Town, Afrika Kusini, akihudhuria Mkutano wa Kwanza wa Uwekezaji wa Maji Afrika. Tukio hili la kihistoria limeandaliwa chini ya uongozi wa Umoja wa Afrika (AU), Jopo la Ngazi ya Juu la Uwekezaji wa Maji Afrika, na Urais wa Afrika Kusini katika Kundi la Nchi 20 (G20).
Mkutano huu umeitishwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini pamoja na Jopo la Ngazi ya Juu la Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika (Africa Water Investment Programme – AIP).
Jopo hili lina Wenyeviti Wenza Watatu: Rais wa Namibia, Rais wa Senegal, na Waziri Mkuu wa Uholanzi. Wajumbe wengine ni Marais wa Afrika Kusini, Tanzania, Kenya, Gambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na Mfalme wa Morocco.
Dkt. Kikwete ni Mwenyekiti Mwenza Msaidizi (Alternate Co-Chair), mwenye jukumu la kuwasaidia Wenyeviti Wenza katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwaka huu, Afrika Kusini ndiyo Mwenyekiti wa Kundi la Nchi 20 (G20).
Viongozi wa Afrika wanaokutana Cape Town kwa sasa wanataka Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika ipewe kipaumbele katika ajenda za mkutano ujao wa G20, uliopangwa kufanyika Novemba 2025 hapo hapo Cape Town.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa katika Mkutano wa Kwanza wa Uwekezaji wa Maji Afrika jijini Cape Town, Afrika Kusini, ulioitishwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini pamoja na Jopo la Ngazi ya Juu la Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika (Africa Water Investment Programme – AIP).

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na viongozi wengine katika Mkutano wa Kwanza wa Uwekezaji wa Maji Afrika jijini Cape Town, Afrika Kusini, ulioitishwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini pamoja na Jopo la Ngazi ya Juu la Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika (Africa Water Investment Programme – AIP).