MSHAMBULIAJI Deus Kaseke aliyekuwa na Pamba Jiji msimu uliyopita ambako alimaliza na bao moja, imeelezwa huenda akajiunga na Singida Black Stars inayonolewa na kocha Miguel Ángel Gamondi aliyewahi kuinoa Yanga.
Endapo hilo likifanikiwa haitakuwa mara ya kwanza kwa Kaseke kuichezea timu hiyo, alikuwepo msimu wa 2021/22 alijiunga nayo akitokea Yanga, baada ya kuachana nao alikaa kwa muda bila timu kabla ya msimu ulioisha kuichezea Pamba.
Chanzo cha ndani kinasema sababu ya kuhitaji huduma ya Kaseke ni kutokana na uzoefu alionao katika Ligi na michuano ya kimataifa, anajituma pamoja na nidhamu inayomsaidia kujipambanua na kuendelea kutunza kiwango chake kwa muda mrefu.
“Hadi sasa mazungumzo yapo vizuri, hivyo kuna asilimia kubwa huenda akawa sehemu ya kikosi chetu, kutokana na nidhamu na kujituma kwake anaweza akawa na wakati mzuri mbele ya kocha Gamondi anayezingatia vitu hivyo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Gamondi ni kocha anayehitaji mchezaji anayejituma kuanzia mazoezini, awe na nidhamu ya kujua anatakiwa kufanya nini na kwa wakati gani, vitu ambavyo Kaseke anavyo, mbali na hilo kipa Metacha Mnata ambaye alimaliza na cleansheets saba msimu uliopita ameongezewa mkataba mpya wa kuendelea kusalia naye.”
Chanzo hicho kilisema Kaseke wakati yupo Yanga ameshiriki katika michuano mbalimbali ya CAF: “SBS tunashiriki michuano ya kimataifa, Kaseke siyo mgeni nayo, alicheza sana akiwa na Yanga pamoja na Taifa Stars, kwa hiyo tumeangalia vitu vingi kutoka kwake.”