Kikwete ahudhuria mkutano wa Uwekezaji wa Maji Afrika

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete  amehudhuria mkutano wa kwanza wa Uwekezaji wa Maji Afrika unaofanyika Cape Town nchini Afrika Kusini. Tukio hilo la kihistoria limeandaliwa chini ya uongozi wa Umoja wa Afrika (AU), Jopo la Ngazi ya Juu la Uwekezaji wa Maji Afrika na Rais wa Afrika Kusini katika Kundi la Nchi 20 (G20).

Mkutano huo umeitishwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini pamoja na Jopo la Ngazi ya Juu la Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika (Africa Water Investment Programme – AIP).

Jopo hilo lina wenyeviti wenza watatu ambao ni Rais wa Namibia, Rais wa Senegal na Waziri Mkuu wa Uholanzi. Wajumbe wengine ni Marais wa Afrika Kusini, Tanzania, Kenya, Gambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na Mfalme wa Morocco.

Kikwete ni Mwenyekiti Mwenza Msaidizi (Alternate Co-Chair), mwenye jukumu la kuwasaidia wenyeviti wenza katika utekelezaji wa majukumu yao. Mwaka huu, Afrika Kusini ndiyo Mwenyekiti wa Kundi la Nchi 20 (G20).

Viongozi wa Afrika wanaokutana Cape Town kwa sasa wanataka Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika ipewe kipaumbele katika ajenda za mkutano ujao wa G20, uliopangwa kufanyika Novemba 2025 hapohapo Cape Town.