Kipigo chawaliza mastaa Afrika ya Kati

KIPIGO cha mabao 2-0 kutoka kwa Madagascar katika mechi za CHAN 2024 kikiwa ni cha tatu mfululizo na kilichoing’oa timu hiyo katika fainali hizo za nane, kimewafanya baadhi ya wachezaji kumwaga machozi na kocha wa timu hiyo amefunguka sababu ya mastaa hao kulia uwanjani.

Jana, Afrika ya Kati inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza ilipoteza mechi ya tatu mfululizo ya Kundi B na kuifanya iwe timu ya pili kuaga baada ya Nigeria iliyopo Kundi D na kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kumwaga machozi mara baada ya filimbi ya mwisho ya pambano hilo.

Hata hivyo, Kocha Sebastian Ngato alisema kilio cha wachezaji kimetokana na uchungu wa kushindwa kupata ushindi katika mechi hiyo muhimu na kuwatupa nje ya michuano mapema.

“Leo (juzi) wachezaji walicheza kwa jitihada na ni makosa madogo dakika za mwisho ndiyo yaliyowaangusha na walitamani kupata matokeo kwa sababu ilikuwa ni Siku ya Uhuru wa Taifa letu,” alisema Ngato na kuongeza;

“Haikuwa bahati yetu katika siku yetu muhimu ambayo licha ya kupoteza mechi za awali, lakini hii dhidi ya Madagascar ulikuwa ni mchezo muhimu kwa ajili ya kufurahi pamoja na wananchi wote wa Afrika ya kati.”

Akizungumzia mechi iliyobaki dhidi ya Taifa Stars inayopigwa kesho usiku, Ngato alisema hautakuwa rahisi kwa sababu wanakutana na wenyeji, pia ndiyo timu iliyofanya vizuri kwa kushinda mechi zote.

“Hatutarajii mteremko, tunatakiwa kujiandaa vizuri ili kukabiliana na timu hiyo ambayo imethibitisha ubora wake kwa kupata matokeo kwenye mechi zao zote walizocheza,” alisema Ngato na kuongeza;

“Mbali na ubora walionao wao wanacheza kwenye ardhi yao ya nyumbani wana watu nje ya uwanja wanawasapoti, ninachosema, maandalizi sahihi tutakayoyafanya ndiyo yatatupa matokeo licha ya kuondolewa kwenye michuano tukiwa na mchezo mkononi.”

Stars inaongoza Kundi B ikiwa na pointi tisa baada ya kushuka uwanjani mara tatu, ikifuatiwa na Mauritania iliyomaliza mechi zake nne ikiwa na pointi saba, kisha Madagascar yenye pointi nne na Burkina Faso itakayovaana na Madagascar kesho pia visiwani Zanzibar ina pointi tatu.