SIMBA ni kama ulivyosikia huko Misri imeshaanza kushusha dozi wakati ikitesti mitambo na habari mpya ni kuongezwa kwa kiungo mwingine ambaye kocha wa timu hiyo Fadlu Davids ameshushiwa kambini.
Juzi, timu hiyo iliisulubu Kahraba Ismailia ya nchini humo kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki ambao chama hilo lilicheza ikiwa ni mara ya kwanza kukipiga kwa mastaa wapya na wale wa zamani katika mchezo dhidi ya timu nyingine, licha ya kwamba haukuwa wa mashindano.
Lakini, kwenye kambi ya Simba kuna kiungo mpya, Naby Camara, aliyeongezwa kwa ajili ya kupimwa na kocha kisha ataamua apewe mkataba mpya au aishie zake.
Unaweza kusema kiungo huyo raia wa Guinea alifika siku nzuri ya shughuli ambapo Simba ikampa nafasi ya kucheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Kahraba Ismailia, ikishinda kwa mabao 2-0 mabao yakifungwa na kiungo Mohammed Bajaber na mshambuliaji Jonathan Sowah.
Camara kwenye mchezo huo alipewa dakika 45 akionyesha kiwango kizuri, akicheza kama kiungo mkabaji kabla ya kubadilishwa na kupumzishwa.
Mwanaspoti inafahamu kuwa Fadlu anataka kuangalia ubora zaidi wa Camara akimpa wiki moja kwenye majaribio hayo sambamba na beki wa kushoto Hernest Malonga, ambaye pia yupo nchini humo tayari.
Kiungo huyo ana mudu kucheza nafasi nyingi kama kiungo mkabaji na beki wa kulia na hata kushoto ambapo kwa sasa hana timu baada ya kuachana na Al Waab.
Camara pia amewahi kuitumikia CS Sfaxien ya Tunisia, kuanzia msimu wa 2019/20 na 2020/21 kabla ya kuachwa na nafasi yake ilichukuliwa na Moussa Balla Conte ambaye ni raia mwenzake wa Guinea.
Fadlu anapasua kichwa namna ya kuunda eneo la kiungo hasa kile cha ukabaji akitaka kumuongezea mtu kiungo wake mpya Allasane Kante, baada ya kumkosa Conte aliyewahiwa na Yanga.
Mbali kiungo mkabaji pia mtihani mwingine wa Fadlu ni namna anavyotafuta beki wa kushoto, akitaka pia kutafuta raia wa kigeni kuja kusaidiana Antony Mligo.
Hata hivyo, kama Fadlu akikubaliana na uwezo wa Camara Simba italazimika kumkata mtu mmoja ili kuingiza jina lake kutokana na tayari ina wachezaji 12 wa kigeni ukiongeza na Neo Maema ambaye atajiunga na timu huyo mara baada ya kumalizika kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN.
Katika nafasi hiyo Simba anacheza Yusuph Kagoma na Kante, huku hatima ya Mzamiru ikiwa bado haijajulikana kama atakwepo msimu ujao.