Safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeiva unaweza kusema hivyo baada ya uwepo wa juhudi mbalimbali za kuwahamasisha Watanzania kuhamia kwenye nishati hiyo salama kimatumizi na kiafya pamoja na haraka.
Leo Alhamisi Agosti 14, 2025 jijini Dodoma kunaendelea hafla ya uzinduzi wa programu ya utoaji majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambayo mgeni rasmi ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko huku likuhudhuriwa na viongozi wa shirika hilo na menejimenti ya wizara.
Hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi za kuhamasisha utumiaji wa nishati safi katika kuhakikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia inakwenda mbele.
Aidha, hatua hiyo ni sehemu ya kuunga juhudi za Serikali ambayo imenuia watanzania asilimia 80 watumie nishati safi ya kupikia ikifika mwaka 2034.
Ikumbukwe, Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema “Sasa tunavyosambaza umeme inabidi ifike mahali umeme huo uwe zaidi ya kuwasha taa na kuchaji simu,” akiwa na maana yapo matumizi mengine ikiwemo kutumika kama nisahti ya mapishi.