Mahakama yaanza kusikiliza shauri la kupinga uchaguzi wa TFF

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeanza kusikiliza shauri la uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), unaotarajiwa kufanyika Keshokutwa Jumamosi, Agosti 16, 2025.

‎Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe hiyo mjini Tanga kwa ajili ya kupata rais wa shirikisho hilo, madai inayowaniwa na rais anayemaliza muda wake, akiwa ni mgombea pekee, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

‎Hata hivyo, uchaguzi huo mpaka sasa uko njiapanda kufanyika, kufuatia mashauri yaliyofunguliwa mahakamani na makundi mawakili tofauti ya mawakili.

‎Miongoni mwa mashauri hayo ni shauri  namba 19873/2025, lililofunguliwa na  mawakili wanne, Aloyce Komba na wenzake watatu, Jeremiah Mtobesya, Deusdedit Luteja na Denice Tumaini.

‎Wajibu maombi katika shauri hilo ni Baraza la Taifa la Michezo (BMT) lenye dhamana ya usimamizi wa michezo yote nchini, ambalo ndilo mjibu maombi  wa kwanza; TFF yenyewe (mjibu maombi wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mjibu maombi wa tatu.

‎Katika shauri hilo lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, wadai wanaiomba mahakama iridhie wafungue shauri la mapitio ya mahakama ili itoe amri kuilazimisha  BMT kutekeleza wajibu wake wa kisheria katika kuisimamia TFF pamoja na mambo mengine, BMT iielekeze TFF kuufuta uchaguzi huo na kuanza upya.

‎Hata hivyo, wakati wakisubiri uamuzi wa maombi yao hayo ya kibali, wanaiomba mahakama hiyo iridhie kutoa amri ya kudumisha hali ilivyo kabla ya siku ya uchaguzi, kusubiri shauri lao kusikilizwa pande zote.

‎Kwa ombi hili ,kama mahakama italiridhia, maana yake uchaguzi huo hautafanyika tarehe hiyo kama shauri hili litakuwa halijasikilizwa.

‎Wajibu maombi wa pili, TFF wameibua pingamizi la awali wakiiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo.

‎Kwa sasa mahakama inasikiliza ombi la waombaji la amri ya kudumisha hali iliyopo, kabla ya kusikiliza pingamizi la TFF.

‎Shauri hili linasikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi mchana huu.

‎Kwa mujibu wa Jaji Maghimbi, kwa kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 16, 2025, basi yuko tayari kuendesha shauri hili mpaka usiku mpaka liishe.