Makundi haya yapo hatarinbi kupata homa ya ini B

Moshi. Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Dk Elichilia Shao amesema zaidi ya asilimia 95 ya maambukizi ya virusi vya homa ya ini aina ya B (Hepatitis B) hutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa.

Dk Shao ameyasema hayo leo, Agosti 14, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusiana na ugonjwa huo ambao umekuwa ni tishio duniani kote.

Amesema ili kupunguza maambukizi ya virusi vya Hepatitis B nchini, kunahitajika jitihada za ziada kuhakikisha wajawazito wanapofika kliniki wanapimwa, ili wale watakaobainika kuwa na maambukizi wapate tiba stahiki, na wasioambukizwa wapatiwe chanjo.

“Ili kuongeza kasi ya kutokomeza maambukizi ya virusi vya Hepatitis B, ni muhimu kuhakikisha kila mjamzito anayehudhuria kliniki anapimwa ugonjwa huo.

“Wale watakaokutwa na maambukizi na kukidhi vigezo wapatiwe matibabu, na wale wasioambukizwa wapewe chanjo. Tukifanikiwa hilo, tunaweza kupunguza maambukizi kwa takribani asilimia 95,” amesema Dk Shao.

Dk Shao amesema tatizo la Hepatitis B ni la kimataifa, ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024, watu zaidi ya milioni 257 duniani wanaishi na virusi hivyo. Hapa nchini Tanzania, asilimia sita ya watu kutoka makundi mbalimbali wanakadiriwa kuwa na maambukizi hayo.

“Hili ni tatizo kubwa, na linahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa mashirika ya Serikali, yasiyo ya kiserikali na watu binafsi. Elimu kwa jamii ni muhimu ili wananchi wapate uelewa, wajitokeze kupimwa, na wahudumiwe kwa wakati.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka utaratibu wa upimaji na utoaji wa matibabu. Kwa wale wasioambukizwa, chanjo ipo na ni salama,” amesisitiza Dk Shao.

Amebainisha kuwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ni pamoja na watoa huduma za afya kutokana na mazingira yao ya kazi, watu wanaojihusisha na biashara ya ngono bila kutumia kinga, wachora tattoo katika mazingira yasiyo salama na watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya sindano.

 “Ugonjwa huu hauambukizwi kupitia jasho wala mate. Mara virusi vinapoingia mwilini, huingia kwenye damu na kushambulia seli za ini. Ini likiathirika huanza kuharibika, kutengeneza makovu na hatimaye linaweza kusinyaa au kugeuka kuwa saratani,” amefafanua Dk Shao.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani yaliyofanyika Julai 28 hospitalini hapo, Dk Shao alisema watu 450 walifanyiwa vipimo vya Hepatitis B na kati yao, asilimia mbili walibainika kuwa na maambukizi.

“Cha kushangaza ni kwamba wote waliobainika kuwa na maambukizi hawakuwa na taarifa kuhusu hali yao. Tuliwapa ushauri, tukawapanga kwenye kliniki zetu kwa ufuatiliaji, na baadhi yao walifanyiwa vipimo zaidi ili kubaini kama wanakidhi vigezo vya kuanza matibabu,” alisema.

Amesisitiza kuwa njia bora ya kutokomeza ugonjwa huo ni kwa jamii kujitokeza kupima afya mara kwa mara ili kubaini hali zao mapema.

“Iwapo kila mmoja wetu atachukua hatua ya kujua hali yake, basi tunaweza kufanikisha lengo la Shirika la Afya Duniani la kutokomeza Hepatitis B ifikapo mwaka 2030,” alihitimisha Dk Shao.