Mji wa Morogoro na viunga vyake umeanza kupendeza juma hili kwa mbwembwe za magari maalumu ya mashindano ambayo yapo mahsusi kwa ajili ya mashindano ya mbio za magari ubingwa wa taifa yanayoanza Jummosi hii.
Mkwawa Rally ndiyo jina la mashindano ambayo yanaanzishwa Agosti 16 na kumalizika Jumapili, Agosti 17.
Klabu ya Mount Uluguru ndiyo waandaaji wa mbio hizo ambazo ni raundi ya tatu ya mbio za magari ubingwa wa taifa kwa mwaka huu, kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu hiyo, Gwakisa Mahigi.
Alisema mbio za Mkwawa Rally zitaanzia uwanja wa Kiwanda cha Tumbaku mjini Morogoro kabla ya kuelekea katika mashamba ya mkonge ya Tumbi.
Hifadhi ya Msitu wa Mkundi, ndilo eneo maalumu la mashindano hayo kwa mujibu wa Mahigi.
Aliongeza kwamba dereva kutoka Iringa, Ahmed Huwel ndiye amepangwa kuondoka wa kwanza katika mbio za magari za Mkwawa Rally.
Huwel ambaye anaingia na gari ya kisasa ambayo ni mahsusi kwa ajili mbio za magari za ubingwa wa dunia (World Rally Championship), atakuwa akiisukuma gari aina ya Toyota GR Yaris ikiwa na namba 10 ubavuni.
Nyuma ya Huwel atakuwapo dereva mkongwe Samir Shanto ambaye ataingia na gari aina ya Ford Fiesta Proto ikiwa na nambari 9 ubavuni.
Wa tatu kuondoka, kwa mujibu wa orodha ya uanzaji ni Randeep Singh ambaye atakuwa akikanyaga ‘eksileta’ ya gari aina ya Mitsubishi Evo 1X akiongozwa na msoma ramani Manmeet Birdi kuusaka ubingwa wa mashindano hayo.
Mshindi wa jumla wa msimu uliopita, Manveer Birdi ataondoka katika nafasi ya nne ndani ya Mitsubishi Evo 1X ikiwa na namba 1 ubavuni akipambana kuhakikisha kwamba anamaliza wa kwanza.
Zubair Piredina ambaye mara nyingi amekuwa akishiriki kama msoma ramani, safari hii anaingia kama dereva akiisukuma gari aina ya Subaru Impreza.
Jumla ya madereva 16 walikuwa wamejiiandikisha kushiriki hadi mwishoni mwa juma na kwa mujibu wa Mahigi, idadi inatarajiwa kuongezeka katika siku tano ziliozobaki kabla ya mashindano kutimua vumbi.