Dar es Salaam. Mtiania wa urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atatumia jukwaa la hotuba baada ya kiapo chake kutangaza kuanza mchakato wa Katiba mpya na kuwashughulikia wabadhirifu papo hapo.
Mpina amesema suala la kukomesha ufisadi halitahitaji subira katika Serikali atakayoiongoza, kwani atalishughulikia ndani ya saa 24 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa nchi.
Ahadi hiyo inakumbusha kile kilichofanywa na Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ndani ya saa 24 baada ya kuapishwa Januari 25, 2025, alipotia saini amri ya kusimamisha kwa muda wa siku 90 misaada yote ya maendeleo kutoka Marekani, kwa lengo la kufanyia tathmini upya.
Mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, hayati Benard Membe, naye alitoa ahadi kama hiyo ingawa kwa muktadha tofauti. Membe aliahidi baada ya kuapishwa na kutia saini kwa wino mwekundu kuwa Rais, watakwenda Ikulu kusherehekea.
Mpina amesema hayo leo, Alhamisi, Agosti 14, 2025, alipozungumza na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipojiunga na ACT Wazalendo na kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho.
Kuhusu ilani ya uchaguzi ya chama chake, amesema imeahidi kufufua mchakato wa Katiba mpya ndani ya miezi sita, hivyo atakaposhinda na kuapishwa, atatangaza kufufua mchakato huo papo hapo jukwaani.
Amesema atafanya hivyo kwa sababu yeye ni muumini wa Serikali tatu na katiba atakayotaka iundwe itazingatia mfumo huo wa Serikali.
“Mwenyezi Mungu atakaponijaalia hiyo Oktoba nikipata hii nafasi na chama changu kimeelekeza kwamba, ndani ya miezi sita mchakato uwe umeanza. Mimi nitaagiza jukwaani pale baada ya kuapa mchakato uanze,” amesema Mpina.
Uamuzi kama huo, ameahidi kuufanya dhidi ya wabadhirifu wa mali za umma na mafisadi, akisema katika jukwaa la hotuba ya baada ya kiapo atawashughulikia.
Amesisitiza kazi ya Rais ni kusimamia sheria na kuhimiza utekelezaji wake, akisema haitakuwa tabu kwake kuelekeza hatua zichukuliwe dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na ubadhirifu wa mali za umma.
Mpina, aliyekuwa Mbunge wa Kisesa kwa miaka 10, amesema Serikali yake itaamini katika kudhibiti ubadhirifu na kuziba mianya ya upigaji kama njia ya kujenga uchumi wa nchi na kulinda rasilimali za asili.
Pia, amesema ndani ya Serikali yake, iwapo atachaguliwa, hakutakuwa na uonevu dhidi ya raia, huku akiahidi kuruhusu uhuru na haki ya kuabudu, kuishi na uhuru wa vyombo vya habari.
Hata hivyo, amesema ACT Wazalendo kimejipanga kwa mipango halali ya kuhakikisha kinapata fedha kwa ajili ya shughuli za kampeni ili kupata ushindi katika kiti cha urais, wabunge na madiwani.
Amevisihi vyama vingine vya upinzani kuunganisha nguvu dhidi ya CCM, ili kukishinda chama hicho tawala na hatimaye kuunda Serikali.
Sababu kujiunga ACT Wazalendo
Mbali na hayo, Mpina amesema amejiunga na ACT Wazalendo baada ya kujiridhisha kuwa chama hicho kinatoa jukwaa madhubuti la kufanikisha ajenda ya vizazi vijavyo na ukombozi wa Taifa.
“Hata kabla sijajiunga na ACT Wazalendo, watu wanaumiza kichwa wanachambua wanatoa ushauri wa kitaalamu. Ni chama ambacho nimekuwa nikikifuatilia. Nipo kwenye chama makini na jukwaa sahihi la kuwakomboa wananchi,” amesema.
Mpina amesema uamuzi wake wa kuhama CCM ni kwa sababu kimepoteza dira na misingi iliyoasisiwa na waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Hata hivyo, Mwananchi iliwatafuta viongozi wa chama hicho, simu zao ziliita bila kupokelewa. Miongoni mwa waliotafutwa ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shamsa Seif ambaye baada ya kuulizwa swali, simu yake ilikatika.
Mpina amesema licha ya kuzaliwa katika familia iliyoota mizizi ya CCM tangu TANU, ameona chama hicho kimepoteza dira na kuondoka katika misingi yake na kimeasi mapambano.
Amesema hayo yamesababisha kuzorota kwa huduma za jamii na hatimaye maadui watatu, umaskini, maradhi na ujinga, wameendelea kushamiri.
“CCM hii sio ile iliyohubiri ukombozi, sio ile ya wakulima na wafanyakazi, kama wenyewe walivyosema kuwa CCM ina wenyewe na wenyewe mmewashuhudia katika harambee yao,” amesema.
Kwa upande wa mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Fatma Alhabib Fereji, amesema anaamini atashirikiana na Mpina, ambaye si mgeni wala jina lake sio jipya na sifa zake za kiuongozi hazihitaji maelezo mengi.
Amesema ameshuhudia miaka 20 ya dhamira ya kweli ya Mpina katika kuwatetea, kuwasikiliza na kutafuta suluhu ya changamoto za wananchi.
“Mpina ni chuma tena chuma kipya kabisa. Chuma kisichonyauka, wala kupauka katika kupigania haki na ubadhilifu wa mali za umma,” amesema.
Ameeleza yaliyomkuta Mpina si ajali ya kisiasa, bali mapenzi ya Mwenyezi Mungu kumuunganisha na chama hicho cha ACT Wazalendo na hatimaye kuwa mgombea wa urais.
“Maono ya kisiasa ya Mpina yamepata jukwaa sahihi kwani ACT Wazalendo ni nyumba ya watu wanaodai haki. Mpina ni kiongozi imara kwenye kulinda maslahi ya watu,” amesema Fatma.