Mrithi wa Anthony Mligo huyu hapa

UONGOZI wa Namungo FC, uko katika mazungumzo ya kuipata saini ya beki wa kushoto wa kikosi cha KVZ ya visiwani Zanzibar, Ally Saleh Machupa ‘Machupa JR’, ili kuziba nafasi iliyoachwa na nyota mwenzake, Anthony Mligo aliyejiunga na Simba.

Mligo aliongeza mkataba wa mwaka mmoja wa kukitumikia kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, japo baada ya Kocha wa Simba, Fadlu Davids kuvutiwa na uwezo wake alipendekeza asajiliwe haraka, hivyo uongozi wa Namungo kuhamishia nguvu kwa Ally.

Mabosi wa Namungo wanamuona Ally ni mbadala sahihi wa kuzipa pengo la Mligo na kwa sasa mazungumzo kati ya mchezaji na Klabu ya KVZ yanaendelea vizuri, ili kuichezea Ligi Kuu Bara msimu ujao akiwa na kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, aliliambia Mwanaspoti kama kuna taarifa juu ya suala hilo, watazitolea ufafanuzi kwa mashabiki zao, japo kwa sasa wanaendelea na maboresho ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao.

“Wachezaji wote tutakaofikia makubaliano nao tutawatangaza katika kurasa zetu rasmi za mitandao ya kijamii, muda wowote kuanzia sasa tutaanza kutangaza mmoja baada ya mwingine hivyo, mashabiki zetu watarajie mambo makubwa,” alisema Ally.

Mbali na Ally, nyota wengine waliojiunga na kikosi hicho ni Cyprian Kipenye (Songea United), Abdulaziz Shahame (TMA FC), Lucas Kikoti (Coastal Union), Heritier Makambo (Tabora United), Abdallah Mfuko (Kagera Sugar) na Jackson Shiga (Fountain Gate).