Mto wachepushwa ujenzi tuta la kufulia umeme Malagarasi

Dar es Salaam. Wakati ujenzi wa bwawa la kufua umeme kwa maji kupitia mto Malagarasi ukifikia asilimia 10, wajenzi wa mradi huo wamechepusha maji (kutengeneza njia ya maji) ili kuruhusu ujenzi wa tuta kuu litakalotumika katika ufuaji wa umeme wa megawati 49.5.

Ujenzi wa mradi wa Malagarasi unatekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambapo ulianza Aprili 10,2024 na unatarajia kukamilika Oktoba 10, 2027, huku gharama za ujenzi wa  mradi bwawa zikiwa ni Sh300 bilioni.

Akizungumza katika hafla fupi ya uchepushaji maji, Jumatano Agosti 13, 2025 Meneja wa mradi Mhandisi Saidi Kimbanga amesema maana nzima ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme inahitaji kuweka utaratibu wa maji kupita katika njia maalumu ili yaweze kufua umeme, ambayo ni hatua muhimu.

 “Ujenzi wa mradi unaenda kwa kasi, uchepushaji maji ulitakiwa kufanyika Agosti 27, lakini tumefanikisha zoezi hili leo, siku zaidi ya 10 nyuma, hivyo tunatarajia utakamilika mapema zaidi,” amesema Mhandisi huyo.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kigoma,  Mhandisi Julius Sabu, ameeleza kwamba kukamilika kwa mradi kutaongeza umeme katika mkoani humo , akiwaalika wawekezaji kutumia fursa hiyo kuwekeza.

Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa iliyokuwa inatumia umeme unaozalishwa na majenereta kabla ya kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Septemba 19, 2024 akiwa mkoani Kigoma wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa uzalishaji umeme katika mto huo pia uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV132 kutoka Igamba hadi Kidahwe na Kituo cha kusambaza umeme msongo wa kV 400/220/132/33 cha Kidahwe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema Serikali ilikuwa inapata hasara kununua mafuta ya jenereta kuzalisha umeme.

Alisema Serikali inatumia Sh35 bilioni kila mwaka kununua mafuta kwa ajili ya majenereta, wakati makusanyo ya Tanesco kwa Mkoa wa Kigoma yanafikia Sh16 bilioni, hali inayosababisha hasara.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu juu ya tija ya mradi huo, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Mwinuka Lutengano amesema nishati ya umeme inazalishwa kutoka vyanzo tofauti. Gharama za uzalishaji na uendelevu wa upatikanaji wa nishati hiyo haufanani kutokana na aina ya chanzo.

“Ukanda huu wa mikoa mfano Kigoma na Kagera, kumekua na changamoto ya nishati ya umeme ya uhakika. Umeme wa mafuta mazito una gharama kubwa.

“Hivyo, kukamilika kwa mradi huu kwa wakati kutaleta chachu muhimu ya uwepo wa umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani, viwandani na hata kwenye biashara ndogo, za kati na kubwa,” amesema Dk Lutengano.