RC ARUSHA AITA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA MBIO ZA MERU FOREST ADVENTURE RACE 2025


Na Pamela Mollel,Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Laban Kihongosi, ametoa wito kwa wananchi wa Arusha na wageni mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki na kutumia fursa zinazopatikana kupitia mashindano ya Meru Forest Adventure Race 2025.

Akizindua msimu wa tatu wa mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika hifadhi ya Napuru, eneo la utalii wa ikolojia nje kidogo ya Jiji la Arusha, Mhe. Kihongosi amesema matukio kama hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kusisimua uchumi wa wananchi mmoja mmoja pamoja na uchumi wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla.

“Tunapopokea wageni kuna fursa nyingi za kiuchumi tunapata. Wageni watalala kwenye hoteli zetu, wenye hoteli watapata kipato, wafanyabiashara watauza mboga na vyakula, maana yake ni fursa kwa wananchi wengi ndani ya Mkoa wetu kwani hata magari yatasafirisha watu pia na hivyo kuwa fursa ya kiuchumi kwa wasafirishaji,” amesema Kihongosi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Msitu wa Meru/Usa (Meru Forest), Bw. Ali Maggid, amesema mashindano hayo yameendelea kukua mwaka hadi mwaka ambapo msimu wa kwanza yalihusisha washiriki 300, msimu wa pili washiriki 500 na kwa mwaka huu makadirio ni zaidi ya washiriki 700.

Ameongeza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri huku burudani, mbio nyingine na zawadi mbalimbali zikiwa zimeongezwa ili kuvutia washiriki wengi zaidi.