Unguja. Mtiania kugombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Said Soud Said amesema iwapo akipata ridhaa ya kuongoza nchi hiyo, vijana wote wa Zanzibar wataoa bure na mahari zao zitalipwa na Serikali.
Pia, amesema atapiga marufuku kutengeneza vitanda vyenye ukubwa wa futi ya sita kwa sita badala yake mafundi watapaswa kutengeneza vyenye ukubwa wa futi tatu kwa nne ili kuongeza kizazi.
Soud ametoa kauli hiyo leo Agosti 14, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ofisi ya chama hicho Mwera Unguja Zanzibar, alipokuwa akieleza nia yake ya kuwania nafasi hiyo na kutangaza sera zake ambazo amesema iwapo wananchi wakimuamini anakwenda kuleta mabadiliko makubwa kuanzia atakapoishia Rais Hussein Mwinyi.
“Vijana wote wataoa kwa pesa za Serikali, hakuna kijana atakayetoa mahari yake. Serikali ina fedha nyingi mpaka inafikia hatua ya kuibiwa, mimi kwa nini nisichukue fedha ile nikawapa vijana kwamba Sh1 bilioni hii, kila mfungo saba, au mfungo mosi, au mwezi wa Shaaban chukua mkaoe ili kuepuka ubakaji,” amesema
Kuhusu hoja ya kuongeza uzazi, Soud ambaye amegombea zaidi ya mara tatu katika nafasi hiyo, amesema; “Nitakapopata nafasi ya urais, nchi hii haitakuwa na vitanda vya sita kwa sita, havitazidi futi nne”
Amesema; “unapokimbia kuzaa ni kule kukaa sita kwa sita, baba yupo huku mama yupo kule, huzai, utasikia ooh hajazaa huu ni mwaka wa tatu, kitanda cha sita kwa sita utazaa vipi?
Soud ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Taifa amesema; “Wazee wetu zamani walikuwa kitanda cha futi mbili na nusu, imezidi sana tatu, na ndio maana walikuwa wanazaa, leo Wazanzibari hatuzaani kisa sita kwa sita, nikipata nafasi mafundi wa sita kwa sita watabadilisha mwelekeo, lazima watu watengeneze kitanda ambacho mwanamke na mwanaume watakaribisha uzazi wa mara kwa mara.”
Pia katika sera zake, amesema iwapo akichaguliwa kushika wadhifa huo, watu watalewa kwa leseni ili kuepusha kufanya mambo ya ajabu, pia askari wapate nafasi ya kuwalinda vizuri na kuwapeleka majumbani mwao au kuwalinda mpaka pombe ziishe waende nyumbani kwao wenyewe.
“Hii itajenga nidhamu ya Zanzibar, haiwezi tu kisa mtu ana fedha yake akaenda kulewa kisha anapita anatukana ovyo tu eti kisa ana fedha, hakuna, nchi lazima kwenye nidhamu na nidhamu inatengenezwa na Wazanzibari wenyewe sio Serikali, Serikali yenyewe ni kusimamia tu,” amesema.
Soud amesema iwapo mtu akikamatwa amelewa bila leseni atapelekwa chuo cha mafunzo (magereza) kwa kipindi cha miezi mitatu ili akajirekebishe na akitoka huko atajua kulewa kwa nidhamu.
Kuongeza mishahara kidiplomasia
Amezungumzia hoja nyingine kwamba ataongeza mishahara kila mwaka lakini Serikali yake haitatumia utaratibu wa kutangaza kwenye majukwaa, kwani kufanya hivyo kunasababisha kuongezeka kwa gharama za maisha maana vitu vinapanda bei.
Badala yake atapandisha mishahara kwa njia za kidiplomasia kwa kupeleka taarifa hizo kwenye ofisi za wafanyakazi.
“Nyongeza ya mishahara itakuwepo kila mwaka hata kama itakuwa ni Sh5,000 lakini itaongezwa ili kodi inayokusanywa na Serikali lazima irudi kwa wafanyakazi kwa utaratibu maalumu,”
Kada nyingine iliyoguswa ni waandishi wa habari iwapo akiingia madarakani watapatiwa bajaji za kubeba watu sita ili wasiwe wanachelewa kwenye majukumu yao.
Hata hivyo, Soud amesema bado kuna kazi kubwa kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani iwapo hakutakuwa na muungano wa vyama vya siasa kwa sababu tayari chama hicho kimeshatengeneza mizizi mikubwa.
Abadili gia angani kura ya mapema
Kuhusu kura ya mapema, Soud ambaye amewahi kupeleka kesi mahakamani kupinga Zanzibar kupiga kura mara mbili, amesema kwa kuwa sheria haijabadilishwa hawana budi kukubaliana na utaratibu huo kwa sasa ili Baraza la Wawakilishi lijalo ndio litakuwa na uwezo wa kubadilisha sheria hiyo.
“Ukweli ni kwamba hoja hii itaendelea kuwepo kikubwa tukubali kwa sasa Wazanzibari kupiga kura katika mazingira haya, ni aibu kubwa watu kufa kisa kupiga kura kwa nchi kama Zanzibar yenye watu wachache kiasi hiki, angalau kuna mazingira ya demokrasia yanaonekana,” amesema
Wakati Soud akisema hivyo, hivi karibuni Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilieleza msimamo wa sheria ya uchaguzi inayotaka Zanzibar kuwa na kura ya mapema na hivyo mpaka sasa hakuna sheria nyingine, hiyohiyo ndio itakayotumika katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Mkurugenzi wa ZEC, Idarous Faina alisema sheria hiyo namba nne ya mwaka 2018 ndio itakayotumika na inawatambua watendaji wa shughuli za uchaguzi, wasimamizi na walinzi wa shughuli hiyo kupiga kura ya mapema ili kuwapa fursa kushiriki katika mchakato huo.
Hata hivyo, Chama cha ACT Wazalendo nacho kimekuwa kikipinga utaratibu huo kikisema hakipo tayari kuona jambo hilo linajitokeza katika uchaguzi huu badala yake kura zote zipigwe siku moja.