Samia atoa ahadi nono, akiweka historia nishani ya CISM Afrika

RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kuwa kiongozi mwanamke wa kwanza na Afrika kutunukiwa nishani ya heshima ya juu ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM), akiahidi kuendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya michezo.

Mbali na nishani hiyo ya juu ya heshima, Rais Samia pia alitunukiwa tuzo ya uanachama wa heshima ya baraza hilo na ngao ya heshima aliyokabidhiwa na Meja Jenerali Maikano Abdullahi wa Nigeria ambaye ni mwakilishi wa Rais wa CISM, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Tangu mwaka 1952, inaelezwa viongozi wa nchi sita pekee za Afrika ndio wamewahi kutunukiwa nishani hiyo, Rais Samia akiwa ni wa saba na kiongozi pekee mwanamke katika historia hiyo.

Akizungumzia heshima hiyo, Rais Samia amesema ni heshima kwake, jeshi la Wananchi na Taifa la Tanzania akibainisha kuipokea kwa moyo wa shukrani huku akitambua hiyo si si heshima ya mtu mmoja bali ni matokeo ya mshikamano.

Rais Samia, alilishukuru baraza hilo kwa kufanya mkutano mkuu wa 79, amesema CISM ni daraja linalounganisha majeshi kupitia michezo, ikiweka mbele misingi ya urafiki, uaminifu na kushindana kwa heshima.

“Kubwa zaidi, kama mnavyoelewa bara la Afrika tuna ajenda yetu ya ‘silence the gun’ ya kunyamazisha bunduki kulia hovyo, jukwaa hili linakwenda kunyamazisha, Ma-CDF (Wakuu wa Majeshi) wanapokutana kwenye michezo wanajenga urafiki,” amesema Rais Samia na kuongeza;

“Ikitokea ni rahisi kuwaambia kuacha kutumia silaha, ku-resolve (kutatua), matatizo yoyote ambayo yanakuja mbele yetu, mazungumzo yanaleta uvumbuzi wa mambo na si silaha wakati wote.”

Akizungumzia ushiriki wa michezo, Rais Samia aliyesimamia Tanzania kuandaa michuano ya CHAN 2024, amesema ni suala mtambuka akiyataka baadhi ya majeshi kushiriki kikamilifu.

“Magereza si kuchunga tu wafungwa muingie kwenye michezo,” amesema Rais Samia na kueleza alivyopokea wito wa Meja Jenerali Maikano Abdullahi aliyeomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Rais Samia amesema nchi inaweza kulitekeleza hilo bila wasiwasi, lakini akaomba muda wa matayarisho.

“Tupeni muda tujiandae na baadaye tutarudi kwenu kusema kwa namna gani, Tanzania ni mwenyeji wa CHAN (Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN), mwaka 2027 tutakuwa wenyeji wa AFCON (Fainali za Mataifa ya Afrika) ninaamini ili pia linawezeka,” amesema.

Rais Samia amegusia suala la uwekezaji wa miundombinu katika michezo na kubainisha lazima liendelee kuwa ni kipaumbele.

“Tumejenga sana mwaka huu sababu ya CHAN na AFCON, tuendelee kuwekeza ili heshima tuliyoipata isitoke tu kwa majeshi,  itoke na pande nyingine,” amesema Rais Samia na kubainisha tuzo hiyo ni ya Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao mshikamano wao umoja na mapenzi yao kwenye michezo ndiyo msingi wa kile kilichofanyika.

Awali Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Stergomena Tax alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa Rais Samia akimtaja kuwa kiongozi wa saba na wa kwanza mwanamke Afrika kuvikwa nishani hiyo tangu mwaka 1952.

Amesema ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya dunia umekuwa na tija akiutaja ushindi wa Tanzania kwenye mashindano ya majeshi katika mbio za nyika za Machi mwaka huu kulililetea heshimia taifa.

“Timu ya wanaume ilikuwa mabingwa na timu yetu ya wanawake ilikamata nafasi ya tatu kati ya mataifa 50 yaliyoshiriki, mafanikio ya michezo yanatoa fursa kwa vijana kuamini michezo ni njia mojawapo kulitumikia taifa kwa weledi na heshima kubwa,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia aliyataja mafanikio ya michezo nchini na kugusia kile inachoikifanya timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), ambayo imetinga robo fainali kwenye CHAN 2014 kwa kuongoza kundi lake.

Akizungumzia vigezo vilivyompa nishani hiyo Rais Samia, Mkurugenzi wa Michezo wa CISM na Mwakilishi Afrika, Kanali Joseph Bakari alisema kwa mujibu wa sheria za baraza hilo, wanaotunukiwa nishani hiyo lazima wajadiliwe na kupitishwa na bodi ya wakurugenzi.

Amesema baada ya kujadiliwa na majina yao kufikishwa kwenye mkutano mkuu na anayepitishwa lazima awe amepata robo tatu ya kura zilizopigwa.

Mbali na Rais Samia, kwa Tanzania pia Rais wa pili, Ally Hassan Mwinyi (sasa ni marehemu) amewahi kupata tuzo hiyo mwaka 1991 Tanzania ilipoandaa mkutano mkuu wa CISM, ikiwa imepita miaka 18 tangu Tanzania kujiunga na Baraza hilo mwaka 1973.