SERIKALI YATOA UNAFUU WA USHURU WA FORODHA KWENYE MALIGHAFI KUUNGA MKONO SEKTA YA UZALISHAJI WA BIDHAA NCHINI.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema serikali imeamua kutoa unafuu wa ushuru wa Forodha kwenye malighafi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ili kuwezesha viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa kwa gharama nafuu na kushindana kwa bei na bidhaa kutoka nje.

Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha bei za bidhaa za ndani zinakuwa shindani sokoni, huku ikiimarisha uzalishaji wa ndani na kupunguza uagizaji wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa nchini. “Tunapotoa unafuu wa forodha kwa malighafi, tunahamasisha uzalishaji zaidi nchini. Matokeo yake, uagizaji wa bidhaa kutoka nje unapungua, matumizi ya fedha za kigeni yanapungua, na ajira zinaongezeka,” alisema Bw. Awadhi.

Kwa mujibu wake, Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inatoa fursa ya misamaha kwa wazalishaji ili kuongeza tija ya uzalishaji na kupunguza gharama. 


Ameeleza kuwa unafuu huu utasaidia bidhaa za ndani kuuzwa kwa bei nafuu zaidi kuliko endapo msamaha huo usingekuwepo.
Kwa upande wake, Emily Wilson amesema mabadiliko yaliyofanywa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 yamegusa taratibu mbalimbali za forodha, hususan namna mizigo inavyoingia na kutoka nchini. “Kupitia semina zetu, tunawapa maafisa na mawakala wa forodha uelewa wa mabadiliko haya na malengo ya serikali kwa mwaka wa fedha husika. Lengo ni kuhakikisha wote tunakuwa na uelewa wa pamoja na kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato,” alisema.

Naye Allan Maduhu Afisa Forodha Mkuu wa TRA alieleza kuwa lengo la mafunzo yanayotolewa ni kuwafundisha wazalishaji namna ya kujaza taarifa (return) kila robo mwaka, zikionyesha jinsi walivyotumia malighafi walizonufaika nazo kupitia msamaha wa forodha. “Serikali inataka kuhakikisha kuwa msamaha huu una manufaa na kuepusha matumizi mabaya,” alisema.

Washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo wafanyabiashara wa kati, wameishukuru serikali kwa kupunguza kodi na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya msamaha wa forodha. “Zaidi ya msamaha wa kodi, tumepata uelewa wa namna bora ya kufuata mwongozo wa serikali na kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza,” walisema.