Shule yaokoa gharama kwa kutumia nishati safi

Morogoro. Shule ya Sekondari Morogoro imepunguza gharama za matumizi ya nishati kwa zaidi ya asilimia 67 kila mwezi tangu kuanza kutumia gesi badala ya kuni na mkaa Novemba 2024.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 yenye wanafunzi wa bweni 615, awali ilitegemea kuni na mkaa, hali iliyosababisha moshi kudhuru afya za wapishi na kuchafua mazingira.

Kupitia mradi wa nishati safi uliofadhiliwa na Wizara ya Nishati kupitia Mamlaka ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), shule ilianza kutumia gesi na mkaa poa usiotokana na miti, hatua inayolenga kupunguza uchafuzi wa mazingira na kulinda afya za wapishi. Mradi huo ulizinduliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Makamu Mkuu wa Shule, Mwalimu Steven Mworia hivi karibuni amesema mradi huo wenye thamani ya Sh40 milioni uliweka majiko sita ya gesi na mtungi wa gesi kwa matumizi ya miezi mitatu.

“Awali, kununua kuni kwa miezi mitatu tulitumia Sh9 milioni. Sasa, gesi inatugharimu Sh3 milioni. Tumeokoa fedha na muda wa maandalizi ya chakula,” amesema akiisisitiza kuwa mafanikio ya mradi yanapaswa kuwa kichocheo kwa taasisi nyingine kuachana na kuni na mkaa.

Amesema Ewura ilitoa mafunzo ya matumizi salama ya gesi na utambuzi wa hatari kabla ya kuanza na hakuna ajali iliyotokea.

Mariamu Mgonde, mpishi shuleni hapo, amesema mfumo mpya umepunguza uchovu na magonjwa ya kifua na macho.

“Kabla, kuni ziliteseka na moshi mkali unaoumiza macho. Sasa napika kwa muda mfupi, katika mazingira safi na salama, sufuria hazichafuki masizi na naweza kupika aina yoyote ya chakula,” amesema.

Mwanafunzi wa kidato cha sita, Everina Stephano amesema wanafunzi sasa wanapata chakula kwa wakati.

“Zamani tulichelewa vipindi kwa kusubiri chakula, na mara nyingine tulianza masomo bila kifungua kinywa. Sasa tunapata chakula kilichoiva vizuri bila harufu ya moshi,” amesema, akiongeza kuwa mtungi wa gesi umewekewa uzio kwa usalama.

Taasisi kutumia nishati safi

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, amesema hadi Machi 2025, jumla ya taasisi 762 nchini tayari zilianza kutumia nishati safi ya kupikia ili kuepuka madhara ya kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi. Kati ya taasisi hizi, 495 ni za umma na 267 ni za binafsi.

Dk Mpango amezipongeza taasisi zilizotekeleza katazo la kutotumia nishati isiyo safi na kutoa rai kwa taasisi ambazo hazijatekeleza agizo hilo ziendelee kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Habari hizi imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hizi, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.