Tanesco yaanza kwa vitendo matumizi nishati safi ya kupikia

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na mkakati wa miaka 10 kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yenye lengo la kuhakikisha Watanzania wanne kati ya watano wanaitumia ifikapo mwaka 2034, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza utekelezaji kwa vitendo.

Mkakati huo uliozinduliwa Mei 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan unalengo la kumtua mama kuni kichwani ikiwa na maana ya kutumia nishati safi kama gesi na umeme zenye uhakika, usalama wa kiafya pamoja uharaka.

Katika kuhakikisha ajenda hiyo inashika kasi Tanesco imewataka wafanyakazi wake kuwa mabalozi wa kutumia nishati ya umeme kupikia huku ikiwapatia majiko ya umeme wafanyakazi hao wayatumie kupikia, suala litakalobadilisha fikra ya jamii kwamba umeme ni ghali.

Hayo yote yamebanishwa katika hafla ya uzinduzi wa programu maalumu ya utoaji majiko kwa wafanyakazi wa Tanesco kwa bei ya ruzuku, iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma, leo Alhamisi Agosti 14, 2025, huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiwa mgeni rasmi.

Akielezea unafuu wa kutumia umeme kwenye hafla hiyo, Dk Biteko amesema endapo ukitumia umeme kupika chakula cha mlo mmoja unakuwa umetumia chini ya uniti moja, sawa na Sh352 ikiwa ni tofauti na ukitumia mkaa unaouzwa kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000.

 “Kwa sasa Watanzania wanaotumia umeme kupikia ni asilimia 4.2 tu ikiwa ni asilimia ndogo ukilinganisha na idadi hali ya Watanzania wanaotumia umeme kwa sasa.

“Ni kweli usiopingika, kwa historia na mazoea tuliyonayo watu wanaamini kutumia umeme kupikia ni ghali sana, hivyo huikwepa nishati hiyo kwa sababu ya hofu,” amesema Dk Biteko ambaye ni Naibu Waziri Mkuu.

Amesema Watanzania hawana sababu ya kuogopa kutumia umeme kupikia kwa kuwa nishati hiyo ipo ya kutosha, salama na vipo vifaa vinavyotumia umeme kidogo kupika chakula kikaiva kama inavyotakiwa.

Pia, amewataka wafanyakazi wa Tanesco kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia Watanzania pamoja na kwenye utekelezaji wa ajenda hiyo.

“Kila mfanyakazi anapaswa kuwa na aibu kuwa na kuni au mkaa nyumbani kwake kwa ajili ya kupikia. Aone fahari kutumia umeme ili wanapowaambia watu wengine wawe mfano kuishi yale wanayoyazungumza,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Tanesco, Lazaro Twange amesema katika kutekeleza ajenda hiyo Tanesco imezindua majiko ya kisasa yanayotumia umeme mdogo na kuivisha haraka ambavyo wamepewa wafanyakazi ili kuwa mabalozi.

Twange amesema Tanesco wameanza kwa kugawa majiko hayo ya umeme kwa wafanyakazi wa shirika kwa bei ya ruzuku na majiko 11,000 yanatolewa kwa wafanyakazi, huku mkakati ukiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anatumia majiko ya umeme yenye gharama nafuu.

“Nishati safi inasaidia kulinda afya dhidi ya maradhi, lakini pia unapika haraka na unaokoa mazingira, majiko haya tunazindua leo yataokoa gharama kubwa ya matumizi ya nishati,”amesema.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, Balozi Zuhura Bundala amesema lengo la shirika hilo ni kuchangia juhudi za kitaifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kufikia ajenda.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Kupitia mradi huu wananchi wataona Tanesco si shirika tu la umeme bali ni mshiriki hai wa kulinda mazingira kuboresha afya na kuhamasisha maendeleo endelevu.

“Programu hii itahamasisha kutanua wigo kwa wananchi kutumia umeme majumbani na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa hivyo, kupunguza uharibifu wa misitu yetu,” amesema.

Janeth Veso wakati akitoa salamu za wafanyakazi wa Tanesco kwenye hafla hiyo, amesema mpango huo utaongeza morali ya matumizi ya nishati safi lengo ikiwa ni kuwahamasisha na kuwawezesha wafanyakazi wa shirika hilo kutumia umeme uliozalishwa.

“Mpango huu utaongeza uelewa kwa jamii juu ya faida za matumizi ya nishati safi kwa wafanyakazi, pia kuwa mabalozi wa mabadiliko ya tabianchi kupunguza gharama za fedha zinatotokana na kipato cha wafanyakazi,” amesema Veso.