Hanang. Tani 128 za dengu zilizokuwa zikisafirishwa kutokana wilayani Hanang mkoani Manyara kwenye Singida bila vibali vya stakabadhi ghalani zimekamatwa.
Tukio hilo limetokea kwenye geti lililopo kata ya Gehandu mpakani mwa mikoa ya Mara, Singida ikiwa ni operesheni maalumu ya kukagua mazao yasiyopitishwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Teresia Ifaray dengu hiyo hazikupitishwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, Teresia Ifaray (watatu kulia) akiwa na baadhi ya viongozi wa halmashauri hiyo baada ya kukamata shehena ya tani 128 ya mazao ya dengu yaliyokuwa yanapelekwa mkoani Singida. Picha na Joseph Lyimo
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 14, 2025 Ifaray amesema wataendelea kudhibiti mazao yote ambayo yanayotolewa wilayani Hanang’ na kupelekwa mikoa jirani bila kuwa na vibali husika.
“Tumekamata malori manne ambayo yalibeba tani 32 kila moja bila kupitia katika mfumo wa stakabadhi ghalani na tutaendelea kudhibiti kwani hakuna sababu ya kutorosha mazao,” amesema Ifaray.
Mrajisi msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Manyara, Absalom Chelinga amesema kila mdau anapaswa kuona aibu kusafirisha mazao bila kufuata utaratibu husika.
Amesema wafanyabiashara watakaokuwa wanafuata kanuni na taratibu watafanya kazi zao kwa urahisi bila kusumbuliwa na mtu yeyote.

Mkuu wa idara ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa halmashauri hiyo, Daniel Luther amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuzingatia usafirishaji wa mazao ikiwamo kuwa na vibali husika kwa mujibu wa sheria.
Mmoja wa wafanyabiashara waliokamatwa na dengu hizo, Hanis Hamidu amesema hakuna sababu ya kufanya utoroshaji wa kusafirisha mazao bila kufuata utaratibu, hivyo wamefanya makosa.
“Shehena ya mazao yetu ya dengu zimekamatwa kwa makosa yetu wenyewe kwani tungekuwa tumefuata sheria, kanuni na taratibu husika tusingekumbwa na haya yaliyotukuta,” amesema.