BAADA ya uongozi wa maafande wa Tanzania Prisons kukamilisha dili la kocha, Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, tayari harakati za usajili zimeanza na kwa sasa timu hiyo imeanza na mshambuliaji wa kati.
Miongoni mwa mshambuliaji anayekaribia kujiunga na kikosi hicho ni Lucas Sendama ambaye msimu wa 2024-2025, aliichezea Stand United ‘Chama la Wana’, ambayo imempa mkataba mpya wa kuendelea kubakia, ingawa mchezaji anataka changamoto mpya.
Mshambuliaji huyo aliyezichezea pia KenGold, Geita Gold, Biashara United na DTB iliyobadilishwa jina baadaye na kuitwa Singida Big Stars baada ya kupanda Ligi Kuu Bara, amemaliza mkataba wake na Stand na sasa Prisons inakaribia kumsajili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lucas alisema ni muda wa kubadili mazingira kwa kutafuta timu nyingine itakayompa changamoto mpya, japo malengo yake kwa sasa ni kuhakikisha msimu ujao anacheza Ligi Kuu Bara.
“Kama kila kitu kitaenda vizuri basi msimu ujao mashabiki zangu watarajie kuniona nikicheza Ligi Kuu Bara, nashukuru uongozi wa Stand United kwa imani kubwa waliyonipatia, licha ya kutofikia malengo yetu ya kuipandisha timu daraja,” alisema Lucas.
Kwa msimu wa 2024-2025, Lucas aliifungia Stand mabao manne Ligi ya Championship, huku akikiwezesha kikosi hicho pia kumaliza nafasi ya tatu na pointi 61, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar na Mbeya City zilizopanda Ligi Kuu moja kwa moja.
Stand ilipata nafasi ya kucheza ‘Play-Off’ kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara na ilianza kwa kupambana dhidi ya Geita Gold iliyomaliza ya nne Ligi ya Championship na pointi zake 56 na kuiondosha kwa kuichapa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya hapo, Stand ikakutana na Fountain Gate iliyotolewa na Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2 na mechi ya kwanza ya ‘Play-Off’, kikosi hicho kilichapwa mabao 3-1, huku marudiano kikachapwa 2-0 na kuondoshwa kwa jumla ya 5-1.