Tumejiangusha, tumeiangusha nchi CHAN | Mwanaspoti

KWA sasa hapa kijiweni tunaona hadi aibu kuzungumzia fainali za CHAN 2024 maana Watanzania tumeamua kuiangusha nchi yetu kwa kutojitokeza viwanjani kutazama mechi.

CAF walipotupa vituo viwili vya mashindano hayo kwa maana ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na New Amaan Complex kwa Zanzibar walikuwa na sababu moja ya msingi.

Sababu hiyo ni imani Tanzania ni nchi ya kimpira na vaibu la soka ni kubwa hivyo wakitupa mashindano tutayapa hadhi stahiki kwa kujitokeza viwanjani kwa wingi na kushuhudia boli likitandazwa.

Maana mashabiki wanapojitokeza kwa wingi viwanjani inakuwa ni jambo jema kwa vile wadhamini wa shindano husika na CAF wanapata fursa ya kujitangaza tofauti na pale mashabiki hawajitokezi kutazama michezo kwa namba kubwa.

Lakini mambo yamekuwa tofauti kwa vile hatuendi kwa wingi katika mechi zinazochezwa hapa nchini za mashindano hayo kuanzia zile za timu yetu ya taifa, Taifa Stars hadi zile za timu nyinginezo.

Kijiwe kinaamini kwa kuamua kwetu kuzichunia mechi za CHAN 2024, tumeliangusha taifa kwa vile ile taswira iliyokuwa mwanzoni Tanzania ni nchi ya kisoka, inaondoka rasmi katika vichwa vya watu wa CAF na tunaonekana ni mashabiki wa Simba na Yanga tu.

Hili linaweza kusababisha tupoteze fursa ya kuandaa mechi za ufunguzi na fainali katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambazo zitachezwa katika hizi nchi zetu za Tanzania, Kenya na Uganda.

Sisi wenyewe tumejiangusha kwa sababu tukikosa mechi za ufunguzi au fainali katika AFCON 2027, tutakuwa tunajinyima fursa za kiuchumi ambazo tutazipata kwa uwepo wa michezo hiyo mikubwa kwenye mashindano hayo.

Wageni wengi hufika kushuhudia mechi hizo hivyo fedha inaweza kuingia kuingia mauzo ya bidhaa na huduma mbalimbali lakini hata kuitangaza nchi yetu.