Dar es Salaam. Wakati pombe ikitajwa kama moja ya vichocheo vya maradhi yasiyoambukiza, athari zake kwa baadhi ya waajiriwa ni kubwa, wakijikuta wanapoteza ajira.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, matumizi ya pombe kupita kiasi huathiri uwezo wa kufanya uamuzi, kupunguza umakini na kuharibu afya ya akili, hali inayoweza kutafsiriwa moja kwa moja kama tishio kwa ajira.
Baadhi ya waraibu wa pombe wamejikuta katika matatizo yakiwamo ya utoro kazini, kushuka kwa ufanisi, ajali mahali pa kazi na uchelewaji wa mara kwa mara, mambo yanayoweka hatarini ajira zao.
Mbali ya hao, wapo vijana waliogeuka mzigo kwa familia zao kwa kushindwa kuendelea na masomo au kupata matokeo mabaya shuleni na vyuoni kutokana na uraibu wa pombe.
Simulizi za waraibu, wazazi
Stumai Abel, mkazi wa Arusha anasema mwanaye (jina linahifadhiwa) kutokana na uraibu wa pombe alipoteza kazi.
“Alianza kunywa kupindukia, baadaye hata mkewe akamuacha na kilichofuata alipoteza kazi, nilimtibu kwa muda mrefu kwenye sober house baadaye alikaa sawa kutokana na tiba aliyoipata Hospitali ya Taifa Muhimbili,” anasema.
Anna Mwakipesile, mkazi wa Kijichi, Dar es Salaam anasema mwanaye wa kiume wa miaka 28 aliachishwa kazi ya ulinzi kutokana na ulevi.
“Alikuwa mchapakazi, alitutunza vizuri hadi akapata mke na mtoto. Sijui nini kilimsibu akaanza kunywa pombe, akawa hajisikii kwenda kazini, akienda anakuwa amelewa, akaanza kuvaa hovyo mwishoni wakamfukuza,” anasema.
Anasema familia ilimpeleka kwa waganga wa kienyeji wakiamini amerogwa. Pia, walimpeleka kanisani na kwenye ushauri lakini bado hajarudi kwenye hali ya kawaida.
Mzazi huyo anasema mkewe aliondoka na mtoto kwa sababu ya kipigo na kudhalilishwa na mumewe awapo mlevi.
Anaeleza anapokosa fedha hunywa pombe za kienyeji hadi kulala kwenye mitaro na asipokunywa hutetemeka kama vile mgonjwa anayehisi baridi.
Ili kupata fedha, anasema amekuwa akifanya kazi zikiwamo za kuzibua mitaro ya maji machafu na kubeba taka kwa malipo ya Sh2,500 hadi Sh10,000.
Isaya Allen, mkazi wa Buguruni anasema ndugu yao amestaafishwa kazi jeshini kutokana na ulevi uliopindukia, hivyo amerejeshwa kwao mkoani Iringa.
“Ndugu yetu alipokuwa kazini alikuwa analewa, mshahara ukiingia unaishia kwenye madeni ya pombe na wakati mwingine wenzake wanamuibia pasipo yeye kujua kwa sababu ya kutojitambua,” anasema.
Baada ya kupata mafao anasema alinunua nyumba na fedha nyingine alizitumia kwenye ulevi, huku akiwagawia wale waliomsifia.
Kutokana na ulevi, anasema alimpiga mzazi wake kisha akauza nyumba aliyonunua ili kuendela kunywa pombe.
Shaban Jongo (40), aliyekuwa akifanya kazi bandarini anasema rafiki zake ni sababu ya yeye kupoteza kazi kutokana na ulevi.
“Nilipokuwa bandarini kila ikifika jioni tunatoka na marafiki zangu kwenda baa tukiingia tunachafua meza, tuliona ni jambo la kawaida na ikitokea siku hiyo hatujatoka nitatuma mtu aniletee nyumbani kwangu,” anasema.
Kutokana na unywaji pombe hadi usiku wa manane, anasema hakupata muda wa kupumzika, hivyo alikwenda kazini kwa kuchelewa akiwa bado mlevi, ufanisi wake ulishuka akafukuzwa kazi.
Hata alipopata kazi sehemu nyingine, pia aliondolewa kwa sababu aliendelea kuwa mlevi.
“Nimejaribu kuacha nimeshindwa siwezi kabisa kulala bila kunywa, hata nikiumwa huwa nawaambia wanipe bia napona,” anasema akieleza ndugu zake wamejaribu kumsaidia lakini imeshindikana.
Richard Andrew (34) aliyepata tiba katika Kituo cha Bagamoyo Recovery Community anasema: “Nilianza kunywa pombe mwaka 2008 nikiwa kidato cha pili, nikaendelea nayo mpaka kidato cha sita nilipata division 4. Ilikuwa msukumo kutoka kwa marafiki shuleni, nilitumia pombe, bangi baada ya kumaliza nikaanza kuona madhara yake, nimekuwa mraibu.”
Anasema alifika kituoni hapo Aprili 16, 2023 alipata tiba iliyomwezesha kuacha pombe na sasa anaendelea na masomo ya chuo.
Godfrey Mkama, daktari bingwa wa kitengo cha dawa za kulevya na uraibu – Itega katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu anasema wagonjwa 290 walilazwa kutokana na uraibu wa pombe kwa kipindi cha miaka mitano.
Anasema mwaka 2020 walikuwa 43, 2021 (40), 2022 (38), 2023 (74) na 2024 (95).
“Namba inaongezeka, hapa kuna mengi; huenda inatokana na uelewa wa jamii kwamba inajua tatizo hili linatibika Mirembe,” anasema.
Anasema wanaofika kutibiwa na kuondoka kwenye sehemu ya dawa za kulevya na uraibu wa pombe ni takribani 90 kila siku, idadi kubwa ikiwa wanaume kutokana na changamoto za uhusiano, matatizo ya kipato au ajira.
“Pia wanaume kwa sababu ya msukumo wa rika hasa ujana na kuiga au kutaka kujaribu, wapo walioanza kutumia vilevi wakiwa na miaka 15 mpaka 25, wengi wanaanza kutumia wakiwa sekondari na vyuoni,” anasema.
“Lakini kijiografia wengi tunaowapata ni kutoka Dodoma nafikiri kwa sababu ya ukaribu na hospitali, wachache Iringa, Singida na Morogoro na wengine ni nje ya mikoa hiyo.”
Dk Mkama anasema wengi huchagua hospitali wakiamini ni sehemu salama kwao ili kuacha uraibu wa pombe baada ya kupata misaada kutoka kwa wataalamu mabingwa wa afya ya akili na saikolojia.
Mkurugenzi wa Kituo cha Bagamoyo Recovery Community, Salvatory Malai anasema kwa kipindi cha miaka minne tangu kituo kilipoanzishwa, wameshatoa huduma kwa waraibu takribani 300 wa dawa za kulevya wakiwamo 70 wenye uraibu wa pombe.
Malai anasema programu ya uraibu wa pombe ni ya miezi mitatu hadi sita ikihusisha kuondoa sumu ya pombe mwilini na ushauri kutoka kwa wanasaikolojia.
“Akimaliza tiba huwa tunamtafuta kujua anaendeleaje, sasa tunao wanne kituoni wanaendelea na huduma. Maeneo ya Bagamoyo uraibu wa pombe si sana wengi ni wa dawa za kulevya,” anasema Malai.
Dk Mkama anasema mwenye uraibu huitaka pombe kila wakati, hata akiamka cha kwanza anaanza kufikiria kuinywa, hata anapowekewa chakula huona cha kwanza ni pombe.
“Anaanza kuwa na tabia tofauti, kufarakana na familia, wenzake, jamii na ukiangalia huko nyuma hakuwa hivyo. Wengine huingia kwenye wizi ili kupata fedha za pombe au kuuza mali zake na za familia ili akanywe pombe. Pia, makosa ya jinai na kujaribu kutaka kufanya vitu visivyo vya kawaida,” anasema.
“Mfanyakazi anaanza kuwa mtoro ama kutokwenda kazini bila sababu au akaenda kazini lakini bila kuwa na morali ya kazi. Kama ni mwanafunzi hatahudhuria vipindi na katika matumizi ya fedha zinaenda zaidi kwenye pombe, hawezi kununua nguo, kutunza familia, maendeleo, hata kujipenda, asilimia kubwa anafikiria ni pombe.”
Kuhusu ongezeko la uraibu wa pombe katika jamii, anasema wapo ambao huiga, huku wengine wakikata tamaa kwa kutokufanikiwa, hivyo kuingia kwenye ulevi.
Pia, msongo wa mawazo, uuzwaji holela wa pombe mitaani na kwa bei rahisi na ongezeko la aina mbalimbali mpya za pombe.
“Mzazi anatumia kilevi kinapatikana kwa urahisi ndani na baadaye anamtamanisha hadi mtoto anaanza kujaribu angali mdogo, anataka kujaribu baadaye unashangaa ameingia kwenye uraibu,” anasema.
Dk Mkama anasema wapo wenye changamoto ya kisaikolojia ambao hujitibu kwa kwa kunywa pombe kupindukia na mwishowe huingia kwenye uraibu.
Mbali ya hayo, anasema unywaji pombe kwenye sherehe huhamasisha na kuifanya kuonekana kitu cha kawaida na muhimu.
“Watu wapewe huduma za kisaikolojia, wasitumie dawa za kulevya au vilevi kutatua tatizo, pia Serikali idhibiti utengenezaji na utumiaji wa pombe kiholela mtaani,” anasema.
Akizungumzia athari za pombe kiafya, Dk Mkama anasema mnywaji anaweza kupata magonjwa ya akili kama sonona, ambayo ni rahisi mtu kufikiria kujiua au kujaribu kujiua.
Anasema wagonjwa wa aina hiyo huwa wanawalaza ili kuwaweka chini ya uangalizi.
“Pia, wanakuwa na ugonjwa wa akili anakuwa na wasiwasi, imani potofu mwingine anakuwa na mwenza wake muda wote anahisi labda anachepuka, wakati si kweli. Pia, kipindi ambacho mwili umepungukiwa pombe (arosto), anakuwa na hali ya kuchanganyikiwa,” anasema.
Dk Mkama anasema katika kuhakikisha matibabu kwa wagonjwa wengi zaidi, Serikali inajenga kituo cha Taifa (National Rehabilitation Center) kinachotarajiwa kukamilika mwakani.
Katika kituo hicho anasema watapata huduma za kitabibu na kupewa ujuzi baada ya matibabu kwa kuwa, wengi huachana na taaluma zao za awali kutokana na kukosa sifa na vigezo.
“Mfano, alikuwa daktari baadaye akaingia kwenye ulevi akapoteza sifa za udaktari, mtu kama huyu anafaa afundishwe kazi nyingine atakayofanya kuongeza kipato ili ajue pia namna ya kujitegemea baada ya kupona,” anasema.
Hata hivyo, anasema uraibu ni ugonjwa wa ubongo ambao una tabia ya kujirudia kama mhusika atapata vichocheo ambavyo alipata mwanzoni.