Wadau wasisitiza ushirikiano kuchochea maendeleo endelevu

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo nchini wameeleza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwao ili kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora na stahimilivu kupitia teknolojia na sera wezeshi.

Wadau wamebainisha hayo leo Agosti 14, 2025 kwenye mjadala ulioandaliwa na Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa wadau wa sekta mbalimbali katika kuchochea maendeleo.

Mjadala huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, umewaleta pamoja wadau wa sekta tofauti kuangazia fursa iliyopo katika ushirikiano wao unaolenga kuchochea Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) kwa Watanzania.

Akizungumza kwenye mjadala huo, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje kutoka  Vodacom Tanzania, Zuweina Farah amesema kampuni hiyo inashirikiana na wadau wengine kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora.

Amesema Vodacom Tanzania iliwekeza katika teknolojia ya huduma za kifedha kwa njia ya simu ambayo sasa inafanya kazi kubwa kurahisisha maisha ya watu.

“Matokeo ni jambo la muda mrefu. Tunachowekeza leo kinaweza kuzaa matunda miongo kadhaa ijayo,” amesema Zuweina.

Amesema wanashirikiana na wadau wengine kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania.

Zuweina amesema bila ushirikiano haiwezekani kutoa huduma kamilifu kwa wananchi, hivyo Vodacom Tanzania inafanya kazi na sekta tofauti kama vile benki.

“Huduma zetu za kidigitali zimewajengea uwezo wananchi, sasa wanawake wanaweza kuweka akiba, wengine wanaweza kukopa. Tumeboresha na kuwezesha maisha ya Watanzania wa kawaida,” amesema.

Pia, amesisitiza kuwa, jitihada za pamoja kwa kufanya kazi na wadau wengine kunaleta matokeo makubwa na ya haraka na kwamba hayawezi kuletwa na mdau mmoja, hivyo ushirikiano unahitajika.

Kaimu Meneja wa Kitengo cha Ushiriki wa Sekta Binafsi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Crispin Ryakitimbo amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inalenga kupunguza umaskini uliokithiri na kuleta ustahimilivu wa mazingira kupitia ushirikiano wa makundi yote katika jamii.

Amesema Dira 2050 ina nguzo tatu muhimu ambazo ni uchumi shirikishi na shindani, kuwajengea uwezo wananchi na maendeleo ya jamii, pamoja na ustahimilivu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Vitu hivi ni vipaumbele vya Taifa katika namna tofauti kama vile viwanda na biashara, maendeleo ya jamii ambayo yanahusisha afya, elimu, usawa wa kijinsia na utunzaji wa mazingira ili kupambana na umaskini bila kuathiri mazingira yetu.

“Dira 2050 inalenga kupunguza umaskini uliokithiri na kuleta uhimilivu wa mazingira ambayo kwa makusudi unahitajika ushirikiano wa makundi yote katika jamii.

“Dira yenyewe ilikuwa shirikishi, ilihusisha makundi tofauti ya watu kama vijana, wanawake, asasi za kiraia. Huo ndio ushirikiano tangu awali kama tunavyoona kwenye dira yenyewe,”amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa CEO Roundtable of Tanzania, Santina Majengo amesema kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu na vijana ili kuchochea maendeleo endelevu na ushindani wa kiuchumi duniani.

Majengo amesema uongozi wa maadili na ustawi wa Taifa unapaswa kujengwa juu ya msingi wa maendeleo endelevu.

“Hakutakuwa na uendelevu wa biashara kama hautegemei uendelevu wa jumla. Tumeona watu, tumeona sayari na tumeona ustawi. Kila mfumo huu unaweza kuendeshwa na maendeleo ya sekta binafsi,” amesema.

Majengo amesema ukuaji wa muda mrefu unahitaji dira ya kitaifa ya wazi kwa miaka 30 ijayo, itakayoundwa kupitia juhudi za pamoja za viongozi wa sekta, wasomi na vijana.

Hata hivyo, ameonya kuwa mnyororo wa elimu hadi ajira kwa sasa hauko sawa, hali inayosababisha wahitimu wengi wa elimu ya juu kushindwa kupata ajira na kukosa ujuzi unaohitajika sokoni.

Amesisitiza mabadiliko ya mtazamo wa kuthamini elimu ya ufundi sambamba na elimu ya kitaaluma, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa wabunifu na wenye ujuzi wa kiufundi unaohitajika katika soko la ushindani wa kimataifa.

“Vijana wetu wasifikirie fursa zilizopo Tanzania pekee, bali pia katika ukanda, Afrika na duniani kote,” amesema.

Awali, akifungua majadiliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia alitoa wito wa kushirikiana na sekta mbalimbali ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili Tanzania, ikiwamo hatari za mabadiliko ya tabianchi, kidijitali na ya kijamii.

“Tanzania, kama mataifa mengine, inakabiliana na mabadiliko ya haraka ya kidijitali. Pia, tunakabiliana na hatari za tabianchi, kwa wakati mmoja, tunapitia mabadiliko ya kijamii. Changamoto hizi haziwezi kutatuliwa na sekta moja,” amesema Rosalynn.