Wafanyakazi Tanesco mfano matumizi nishati safi ya kupikia

Dar es Salaam. Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange amesema wao kama shirika lazima wawe mfano wa kutumia nishati hiyo salama na muhimu katika kuokoa muda.

Amesema shirika lilifanya utafiti na kubaini kuna vifaa vya kutumia umeme kama majiko janja ambayo yanaweza kupika chini ya uniti moja na chakula kikaiva. Hivyo kwa kuanza na wafanyakazi wa shirika wameamua kuanza safari ya matumizi ya nishati hiyo.

New Content Item (1)

Amebainisha hayo leo Alhamisi Agosti 14, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa programu ya utoaji majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa Tanesco, ambayo mgeni rasmi ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ambapo pia imehudhuriwa na viongozi wa shirika hilo na menejimenti ya Wizara ya Nishati.

Twange anayasema hayo wakati Serikali inaendelea na juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi kufikia ajenda yake ya Watanzania asilimia 80 watumie nishati safi ya kupikia ikifika mwaka 2034.

Hata hivyo, umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme na gesi imetajwa kuwa salama kimatumizi na kiafya kwa kuwa hakuna moshi pamoja na kuokoa muda.

“Sisi kama Tanesco ambao umeme ndio nyumbani lazima tuoneshe mfano kama tunatumia au tunazungumza. Sasa ili tukabane na tuthibitishe tunatumia tumekubaliana wafanyakazi kuwezeshana kama sehemu ya mpango, tutakuwa na uwezo wa kusambaza majiko na kila mtumishi lazima apate jiko akatumie athibitishe uwezo wake na awe balozi,” amesema.

Twange amesema katika kutekeleza ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia wamezindua majiko ya kisasa ambayo yanatumia umeme mdogo na kuivisha haraka, ambayo watapewa wafanyakazi wa shirika hilo ili kuwa mabalozi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Twange amesema kwa kuanza jumla ya majiko 10,000 yatatolewa kwa wafanyakazi wa shirika hilo, huku mkakati ni kuhakikisha kila mwananchi anatumia majiko ya umeme yenye gharama nafuu.

“Nishati safi inasaidia kulinda afya dhidi ya maradhi, lakini pia unapika haraka na unaokoa mazingira, majiko haya tunazindua leo yataokoa gharama kubwa ya matumizi ya nishati.”

Awali, akitoa salamu za wafanyakazi wa shirika hilo,  Janeth Veso amesema mpango huo utaongeza morali ya matumizi ya nishati safi lengo ikiwa ni kuwahamasisha na kuwawezesha wafanyakazi wa Tanesco kutumia umeme uliozalishwa.

“Mpango huu utaongeza uelewa kwa jamii juu ya faida za matumizi ya nishati safi, kwa wafanyakazi pia kuwa mabalozi wa mabadiliko ya tabianchi kupunguza gharama za fedha zinatotokana na kipato cha wafanyakazi,” amesema Veso.

Ikumbukwe, Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema “Sasa tunavyosambaza umeme inabidi ifike mahali umeme huo uwe zaidi ya kuwasha taa na kuchaji simu,” akiwa na maana yapo matumizi mengine ikiwemo kutumika kama nishati ya kupikia.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Balozi Zuhura Bundala amesema lengo la shirika hilo ni kuchangia juhudi za kitaifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia ajenda ya Watanzania asilimia 80 watumie nishati safi ya kupikia ikifika mwaka 2034.

Hivyo shirika hilo linataka kubadilisha fikra kwa jamii kwamba umeme ni matumizi yaliyozoeleka bali hata kupikia kwani kuna vifaa vya kupikia vinavyotumia umeme kidogo. “Ndio maana wamekuja na programu ya ugawaji majiko kwa wafanyakazi wa shirika hilo itakayosaidia kwanza kubadili fikra ya jamii kwa kuona wanachofanya Tanesco.”

“Kupitia mradi huu wananchi wataona Tanesco si shirika tu la umeme bali ni mshiriki hai wa kulinda mazingira kuboresha afya na kuhamasisha maendeleo endelevu. “Programu hii itahamasisha wananchi kutanua wigo wa kutumia umeme majumbani na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kupunguza uharibifu wa misitu yetu,” amesema.

Endelea kufuatilia Mwananchi