Njombe. Viongozi na wajumbe 30 kutoka Kijiji cha Ngwala kilichopo Wilaya ya Songwe mkoani Njombe wamekwenda wilayani Ludewa kwa ajili ya kujifunza mbinu bora za matumizi ya fedha zilizopatikana kutokana na fidia ya mradi wa Liganga na Mchuchuma.
Viongozi hao wamekwenda kujifunza hayo kupitia mafanikio yaliyopatikana katika Kijiji cha Mundindi ambapo kiliwakatia kuwakatia bima ya afya wananchi wake huko wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Ziara hiyo imekuja kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la Machi 11, 2025 ambapo alihimiza kuwa fedha za fidia zitumike kuchochea maendeleo ya wananchi.
Akizungumzia uzoefu wao leo Agosti 14, 2025, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratias amesema baada ya kupokea fidia ya mradi wa Liganga na Mchuchuma, uongozi wa halmashauri na Kijiji cha Mundindi ulikaa na kukubaliana kuhamasisha wananchi sehemu ya fedha hizo kuwekeza katika hati fungani.
Amesema kijiji hicho kilipokea zaidi ya Sh460 milioni kama fidia baada ya kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma, kisha kuweka hatifungani ya Sh400 milioni ambapo kupitia usimamizi wa halmashauri na viongozi wa kijiji hicho, faida iliyopatikana kutokana na gawio waliwakatia bima za afya wananchi wote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratias akizungumza na viongozi na wajumbe kutoka Kijiji cha Ngwala mkoani Songwe waliofika wilayani humo kujifunza namna kijiji cha Mundindi kilivyotumia fedha za fidia kuwakatia bima wananchi wao
Ameongeza kuwa hatua hiyo imeweza kuboresha huduma za afya kwa kiasi kikubwa katika Kijiji cha Mundindi na kuondoa kikwazo cha gharama kubwa za matibabu kwa wananchi wa kijiji hicho.
“Afya ni msingi wa maendeleo ya wananchi, hivyo tulihakikisha fidia hii inagusa maisha ya kila mtu moja kwa moja,” amesema Deogratias.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Dk Twilumba Lihweuli amesema mpango huo umesaidia kuondoa utegemezi wa dawa za asili kutokana na wananchi kukwepa gharama za hospitali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngwala kilichopo mkoani Songwe, Bright Kumwenda amesema wamefika Kijiji cha Mundindi ili kujifunza namna ambavyo wananchi wake walivyonufaika na fedha za kijiji.
“Kwa hiyo tumepata semina na maelekezo mafupi kutoka halmashauri, mkurugenzi ametuelekeza, tumefurahi sana na tukifuata utaratibu huu, kijiji chetu kitanufaika kupitia bima ya afya na watoto watasoma,” amesema Kumwenda.
Akizungumzia hatua hiyo, mkazi wawa Kijiji cha Mundindi, Clementina Mkinga, aliyesema bima hizo za afya zimeondoa hofu ya kuumwa na kushindwa kupata matibabu hospitalini kutokana na kukosa fedha.