Dar es Salaam. Mtiania wa urais wa Tanzania wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Gombo amewataka Watanzania kuacha kulalamika kuhusu hali ngumu ya maisha badala yake wajitokeze kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, ili kuiweka madarakani Serikali inayowajibika kwa wananchi.
Gombo amewasihi wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kama njia halali ya kuleta mageuzi wanayoyataka. Akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Husna Abdallah Mohamed, walipokelewa na viongozi wa chama hicho wakiwa wamerejea kutoka kuchukua fomu ya kugombea urais kwenye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano wa makada wa chama hicho, Gombo amesema licha ya changamoto zilizopo kwenye Katiba ya sasa, bado inaweka wazi mamlaka ya wananchi kuamua aina ya Serikali wanayoitaka. Amedai Serikali iliyopo imekosa kusikia na kujibu kilio cha watu wa kawaida huku ikiwapa kipaumbele wenye nacho.

“Tusilalamike tufanye uamuzi kimyakimya, mazingira haya hatuwezi kubadilisha Serikali ikiwa tunaendelea kulalamika.
“Haki huwa haiombwi huwa inapiganiwa, tukapige kura zote kwa wingi na zikiwa nyingi watashindwa kuiba watazidiwa na kuona aibu hiyo itasaidia kuweka Serikali tunayotaka na kujibu malalamiko yetu na tugawane keki ya Taifa, kwa uhuru kabisa,” amesema.
Gombo ameahidi iwapo CUF itashinda dola, itatekeleza sera ya afya bure, ajira kwa wote, na haki sawa kwa wananchi, akisema muda wa kuwa na Taifa la watu wanaoombaomba umepita.
“Wenye kuhitaji kuajiriwa wataajiriwa, na hilo litatimia ikiwa CUF itashika dola, hatuhitaji watu kuomba omba iwe mwisho kwani inaleta mazingira ya rushwa.

Kwa kutambua hilo, Gombo amedai ni muhimu kutumia udhaifu wa Katiba iliyopo kuweka Serikali mpya na kuiondoa iliyopo, CCM imekuwa kiziwi haifanyi mambo kwa masilahi ya watu wa chini isipokuwa kina wakumbatia wenye nacho.
“Tunapaswa kuungana kuiondoa Serikali iliyopo madarakani, tuache kulalamika isipokuwa tuchukue hatua, CCM haiwezi kujichongea yenyewe kufanya mabadiliko ya Katiba ili iondoke madarakani katu haiwezi kutokea,” amedai.
Awali, mtiania wa urais wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad amesema kwa muda uliobaki chama hicho kimejipanga afe beki au kipa ni muhimu kwao kuungana ili wakashinde dola.
“Wagombea tuko wamoja, wanachama ondoeni wasiwasi, na tunakusudia kwenda Zanzibar kuhakikisha tunashinda, kura zangu zipo Zanzibar wakinipigia nyingi tunashinda,” amesema.
Amesema Zanzibar ni Unguja na Pemba, lakini mapokezi ya wagombea kwa chama hicho, kwa visiwa hivyo yatafanyika Pemba huku akitaka wanachama na makada kujitokeza kwa wingi kuwalaki wagombea hao.
Naye Makamu Mwenyekiti wa CUF Bara, Omar Dunga amesema mwaka huu chama hicho kinashiriki Uchaguzi Mkuu na kushinda, si kwamba wanasindikiza kama wanavyodhania wengi, isipokuwa wamejipanga, wan adhamira na ari ya kwenda kushinda dola ya Tanzania na Zanzibar.
Dunga amebainisha safari ya kuchukua dola hiyo haiwezi kuwa rahisi, wanajua watakumbana na vikwazo vingi kulingana na aina ya mazingira ya demokrasia iliyopo hivyo, wanachama na makada wake wanapaswa kujipanga kisawasawa.
“Tunawaeleza CCM, tumejipanga hivyo na nyie mjipange kisaikolojia kuja kuishi maisha ya mtaani msione…sooo kwani nako mtaani huku kuna maisha, wakati wa kuchezea Ikulu umeisha sasa, mtupishe,” amedai Dunga.
Baada ya kuchukua fomu, Dunga amesema jukumu walilonalo kwa wanachama wote ni kuwaunga mkono kwa kuwadhamini, huku akieleza ni matumaini shughuli hiyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam itakamilika haraka.