Wawili Simba watimkia Yanga | Mwanaspoti

YANGA Princess imekamilisha usajili wa wachezaji wawili kutoka Simba Queens wakiwa ni kiungo Ritticia Nabbosa na beki wa kushoto Wincate Kaari.

Timu hiyo ilimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL) msimu uliopita na kwenye mechi 18 ilishinda 12, sare tatu na kupoteza tatu ikikusanya pointi 39.

Mwanaspoti liliripoti mwezi uliopita timu hiyo iko kwenye hatua za mwisho kumalizana na wachezaji hao walioitumikia Simba msimu uliopita.

Kiongozi mmoja wa Yanga Princess ambaye hakutaka jina litajwe amelithibitishia gazeti hili wameshakamilisha usajili wa nyota hao – Nabbosa akisaini miaka miwili na Kaari mmoja.

Kwa Nabbosa itakuwa mara ya kwanza kuichezea Yanga, lakini Kaari hii ni mara yake ya pili baada ya msimu wa 2023/24 kuwatumikia Wananchi na msimu uliofuata akaibukia Simba.

“Usajili huo umezingatia ripoti ya kocha anayehitaji kuwa na kikosi imara ili kuhakikisha msimu ujao tunafanya vizuri na kunyakua taji kama ilivyo malengo yetu,” alisema kiongozi huyo.

“Mwishoni mwa mwezi huu tunaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na ligi inaweza kuanza mapema, hivyo tunawahi ili kujiweka fiti zaidi.”

Nabbosa, raia wa Uganda ambaye aliwahi kuichezea Fountain Gate, alicheza misimu miwili Simba, lakini uliopita hakupata nafasi ya kuanza mara kwa mara akikumbana na ushindani wa nafasi mbele ya Ester Mayala.

Kwa upande wake Kaari alicheza mechi 16 za Ligi Kuu na inaelezwa hakutaka kusalia Simba licha ya ofa kubwa aliyowekewa.

Huo utakuwa usajili wa nne kwa Yanga msimu huu baada ya ule wa Presious Christopher kutoka Simba na beki wa kati Akudo Ogbonna akitokea IFK Kaimal inayoshiriki Ligi Kuu Sweden.